Dili la Gyokeres sarakasi kibao
Muktasari:
- Gyokeres ataachana na Sporting kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini kinachoulizwa heshima yake itabaki kubwa kwa kiasi gani kwenye klabu hiyo kutokana na vita ya maneno inayoendelea.
LISBON, URENO: SAKATA la straika Viktor Gyokeres kuachana na Sporting Lisbon limechukua sura mpya baada ya mkali huyo wa kimataifa wa Sweden kuwachapa barua ya kisheria waajiri wake.
Gyokeres ataachana na Sporting kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini kinachoulizwa heshima yake itabaki kubwa kwa kiasi gani kwenye klabu hiyo kutokana na vita ya maneno inayoendelea.
Arsenal na Sporting zimefikia makubaliano ya mdomo juu ya dili la Pauni 55 milioni pamoja na nyongeza ya Pauni 8.6 milioni kwa ajili ya huduma ya straika Gyokeres.
Lakini, mkurugenzi wa michezo wa Arsenal, Andrea Berta ameshindwa kufikia makubaliano ya jumla ya kuhusu malipo hayo ya ada.
Jambo hilo limefungua milango kwa Manchester United kurudi kwenye mchakato wa kumnasa straika huyo na wameweka mezani ofa yao kwa ajili ya kuvamia dili hilo.
Ripoti kutoka Ureno zinafichua Man United imeweka mezani ofa yao inayoanzia Euro 70 milioni hadi Euro 80 milioni wakijaribu jambo lao la kumuunganisha Gyokeres na kocha wake wa zamani, Ruben Amorim wakapige mzigo pamoja Old Trafford.
Bado haifahamiki kama Man United inaweza kupindua meza, lakini kitu kinachofahamika kwa hakika ni Gyokeres ameshavunja daraja lake la maelewano na mabosi wa Sporting. Straika huyo mwenye umri wa miaka 27 anachotaka kwa sasa ni kuachana na timu hiyo na hilo limemfanya kuingia kwenye mzozo mkubwa na rais wa Sporting, Federico Varandas.
Gyokeres anadhani alikubaliana na Varandas kumruhusu aondoke endapo kama kutakuwa na timu itakayokuwa tayari kutoa Euro 60 milioni pamoja na nyongeza ya Euro 10 milioni, lakini bosi huyo amekataa ofa kadhaa za aina hiyo.
Gyokeres ameingia kwenye mgomo akikataa kutokea kwenye mechi za mazoezi ya pre-season huko Sporting, akidai hatachezea timu hiyo tena. Sporting ilidai itamchukulia uamuzi wa kinidhamu mshambuliaji huyo.
Na sasa, gazeti la Record linaripoti Gyokeres, kupitia wawakilishi wake wa kisheria, wametuma barua kwa mabosi wa Sporting, ikidai kukosekana kwa mteja wao kwenye mazoezi ya timu hiyo kutokana na makubaliano na Varandas.
Kinachoelezwa ni dili la Gyokeres kwenda Arsenal limekwama kutokana na klabu hizo mbili kushindwa kufikia mwafaka kwenye malipo ya bonasi ya Pauni 8.6 milioni, yalipwe kwa namna gani.