Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Didier Deschamps aaga kwa maumivu

UFARANSA Pict

Muktasari:

  • Deschamps, aliyewahi kutwaa Kombe la Dunia akiwa mchezaji mwaka 1998 na baadaye akiwa kocha mwaka 2018, alikuwa akilenga kuweka historia ya kulinyanyua kwa mara ya tatu. Ndoto hiyo imezimwa na Hispania, huku Ufaransa ikishindwa kabisa kuonyesha ubora wake.

MIAMI, MAREKANI: SAFARI ya Didier Deschamps ndani ya timu ya taifa ya Ufaransa imefika tamati kwa namna ambayo asingependa kuikumbuka. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 57 atamaliza enzi yake kwa mechi ya kusaka nafasi ya tatu kwenye Kombe la Dunia, baada ya Ufaransa kutolewa na Hispania kwa mabao 2-0 katika nusu fainali iliyopigwa jana Jumanne.

Deschamps, aliyewahi kutwaa Kombe la Dunia akiwa mchezaji mwaka 1998 na baadaye akiwa kocha mwaka 2018, alikuwa akilenga kuweka historia ya kulinyanyua kwa mara ya tatu. Ndoto hiyo imezimwa na Hispania, huku Ufaransa ikishindwa kabisa kuonyesha ubora wake.

Licha ya kuingia nusu fainali ikiwa imeonyesha soka la kuvutia la kushambulia, Ufaransa ilipiga mashuti 10 pekee dhidi ya Hispania, idadi ndogo zaidi kwao katika Kombe hili la Dunia. Takwimu zao za mabao yanayotarajiwa zilikuwa 0.3 tu, jambo lililoonyesha jinsi walivyoshindwa kutengeneza nafasi za hatari.

UFA 05

Kiungo wa zamani wa Ufaransa, Patrick Vieira, hakuficha masikitiko yake.

“Ufaransa haikufika kabisa kwenye kiwango kilichotarajiwa. Tulitegemea mengi zaidi. Kulikuwa na matarajio makubwa ya kushinda Kombe la Dunia, lakini wachezaji wetu wakubwa walipotea na kwa ujumla tulikuwa wabovu,” amesema.

Nahodha Kylian Mbappe naye alikiri kuwa walishindwa kutekeleza mpango wao wa mchezo.

“Usipofanya kile unachotakiwa kufanya katika nusu fainali ya Kombe la Dunia, hushindi. Tulitaka kuwabana juu ili wasiweze kutawala mchezo kwa pasi zao, lakini hatukufanikiwa. Wao walikuwa bora kuliko sisi katika kudhibiti mchezo,” amesema.

UFA 01

Ingawa ameondolewa, Deschamps aliweka rekodi mpya ya kuiongoza timu katika mechi nyingi zaidi za Kombe la Dunia. Mchezo dhidi ya Hispania ulikuwa wa 26 kwake, akimzidi Helmut Schon wa Ujerumani Magharibi aliyekuwa na rekodi ya mechi 25.

Deschamps alitangaza mapema mwaka 2025 kuwa angeondoka baada ya Kombe hili la Dunia. Atahitimisha rasmi safari yake kwa mchezo dhidi ya mshindi wa nafasi ya tatu kati ya England na Argentina utakaochezwa Miami.

“Sio wakati wa kuzungumzia maisha yangu ya baadaye. Jambo muhimu ni kile tulichokifanya kwa miaka yote. Najivunia kufikisha Ufaransa katika kiwango cha juu na kushinda Kombe la Dunia. Leo ni siku ya maumivu, lakini haiwezi kufuta yote tuliyoyafanikisha,” amesema.

UFA 03
UFA 03

Kocha huyo ni mmoja wa watu watatu pekee duniani waliowahi kushinda Kombe la Dunia kama mchezaji na kocha, akifuata nyayo za Mario Zagallo wa Brazil na Franz Beckenbauer wa Ujerumani Magharibi.

Katika miaka 14 aliyokaa benchi la Ufaransa tangu mwaka 2012, Deschamps ameiongoza timu hiyo katika mechi 26 za Kombe la Dunia, akishinda 20 na kupoteza tatu pekee.

Pia ameifikisha Ufaransa robo fainali au zaidi katika mashindano manne mfululizo ya Kombe la Dunia, huku mwaka 2022 wakipoteza fainali kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Argentina baada ya kuwa karibu kutetea ubingwa.

Licha ya kuwa na kikosi chenye nyota kama Mbappe, mshindi wa Ballon d’Or Ousmane Dembele na Michael Olise, Ufaransa ilishindwa kufikia matarajio.

UFA 04

Ms hambuliaji wa zamani wa Ufaransa, Olivier Giroud, amesema wachezaji wote walitaka kumpa Deschamps mwisho mzuri.

“Alistahili kuondoka akiwa bingwa, lakini hilo halikutokea. Hata hivyo, mafanikio yake kwa miaka 14 yanajieleza yenyewe. Kwetu baadhi ya wachezaji alikuwa kama baba wa pili. Alitupa imani kubwa na ndiyo maana tutabaki tumefungwa naye milele baada ya kushinda Kombe la Dunia mwaka 2018,” amesema Giroud.

Giroud ameongeza kuwa Deschamps aliwapa wachezaji uhuru mkubwa uwanjani huku akisisitiza nidhamu na uwiano wa timu.

“Kitu kikubwa alichotufundisha ni ushindani. Alitaka tushinde kila mchezo na alitufanya tuamini hilo kila wakati,” ameongeza.

UFA 02

Beki wa zamani wa Ufar ansa, Arsenal na Manchester City, Gael Clichy, naye amesema Deschamps ameibadilisha kabisa sura ya timu ya taifa.

“Aliikuta Ufaransa ikiwa kwenye hali mbaya baada ya kushindwa kwenye mashindano kadhaa, lakini akairejesha kileleni. Hicho ndicho kitakachobaki kuwa urithi wake mkubwa,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, nguli wa soka la Ufaransa, Zinedine Zidane, ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kumrithi Deschamps. Zidane, aliyeshinda Kombe la Dunia la 1998 pamoja na Deschamps na baadaye kutwaa mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa kocha wa Real Madrid, anaripotiwa kuwa tayari amefikia makubaliano ya awali ya kuichukua timu hiyo.

Hata hivyo, Clichy anaamini kazi inayomsubiri kocha atakayekuja haitakuwa rahisi.

“Atakayekuja baada ya Deschamps atakuwa na kazi ngumu sana. Si rahisi kurithi mafanikio makubwa kama haya,” amesema.