Dembele ndiye mchezaji bora wa mwaka wa Fifa
Muktasari:
- Kwenye mchakato huo, Dembele amewabwaga mastaa wawili, Kylian Mbappe wa Real Madrid na Lamine Yamal wa Barcelona.
DOHA, QATAR: STAA wa Paris Saint-Germain, Ousmane Dembele amechaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Fifa kwa 2025.
Kwenye mchakato huo, Dembele amewabwaga mastaa wawili, Kylian Mbappe wa Real Madrid na Lamine Yamal wa Barcelona.
Ushindi huo wa Dembele, 28, unakuja baada ya kuwa na mwaka bora kabisa akishinda mataji ya Ligue 1, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Coupe de France akiwa na kikosi cha miamba hiyo ya Parc des Princes.
Dembele, ambaye ni supastaa wa kimataifa wa Ufaransa aliisaidia PSG ya kocha Luis Enrique kufika fainali ya Kombe la Dunia la Klabu, Julai mwaka kubeba UEFA Super Cup msimu huu. Kiwango bora cha uwanjani cha Dembele kilimfanya ashinde pia Ballon d'Or, Oktoba mwaka huu, ikiwa ni tuzo binafsi ya thamani ya juu kabisa katika mchezo wa soka.
Katika sherehe za tuzo za Fifa zilizofanyika Jumanne huko Doha, Qatar, Dembele aliibuka tena mshindi mbele ya Mbappe na Yamal waliokuwa wametinga kwenye tatu bora.
Rais wa FIFA, Gianni Infantino alimtangaza Dembele kuwa mshindi huku tukio la upigaji kura lilifanyika kati ya Agosti 11, 2024 na Agosti 2, 2025. Ndani ya muda huo, Dembele alifunga mabao 35 na kuasisti 14 akiwa na PSG.
Dembele alishindwa kuisaidia timu yake ya taifa ya Ufaransa, Les Bleus kwenye mashindano ya Nations League, ambapo yeye na Mbappe walipoteza kwenye hatua ya nusu fainali mbele ya Hispania ya Yamal.
PSG ipo huko Qatar kwenye mashindano ya Intercontinental Cup, ambako Jumatano ilitarajia kukipiga na Flamengo.
"Nataka kuwashukuru wachezaji wenzangu," alisema Dembele, 28, akiwa na tuzo yake mkononi.
"Kupambana kunalipa, umekuwa mwaka mzuri kwangu, kama mchezaji binafsi na kwa timu kwa ujumla."
Kwenye sherehe hizo kulitajwa pia Kikosi Bora cha Mwaka cha Fifa; Gianluigi Donnarumma; Achraf Hakimi, Willian Pacho, Virgil van Dijk, Nuno Mendes; Cole Palmer, Jude Bellingham, Vitinha, Pedro; Lamine Yamal, Ousmane Dembele.
TUZO ZILIZOTOLEWA NA FIFA KWENYE SHEREHE HIZO
Mchezaji bora wa kiume: Ousmane Dembele
Mchezaji bora wa kike: Aitana Bonmati
Kocha bora wa kiume: Luis Enrique
Kocha bora wa kike: Sarina Wiegman
Bao bora la mwaka: Santiago Montiel (Independiente vs Rivadavia)