De Gea atoa gundu la penalti

Sunday September 19 2021
de gea pic

LONDON, ENGLAND. NDIOO. Baada ya miaka, miezi, wiki, siku, saa na sekunde hatimaye golikipa wa Manchester United na Hispania, David de Gea amefuta rekodi mbaya ya kuwa shati kila lilipokuja suala la kupigiwa penalti kwenye lango lake akiwa na timu ya taifa na klabu.
Hiyo ilikuwa ni baada ya wiki  kuanza vibaya kwa vijana wa Jiji la Manchester na leo wameibuka na ushindi  wa mabao 2-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi West Ham.
Man United ilipata ushindi kwenye mchezo huo  mgumu uliokuwa na purukushani nyingi zilizosababisha hadi kufikia dakika ya 88 ubao kusoma bao 1-1.
Ilikuwa ni Lingard aliyepiga shuti kali dakika ya 89 ikiwa ni muda mchache baada ya kuingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya Paul Pogba.
Lakini bao hilo liliingia kwenye hati hati yakuwa kazi bure baada ya Luke Shaw kushika kwenye eneo la boksi hali iliyosababisha aliyekuwa mwamuzi wa mchezo huo  Martin Atkinson kwenda kuangalia kweye VAR na kuamua kwamba ilikuwa ni penalti iliyokwenda kupigwa na Mark Noble, lakini mwanajeshi wa mchezo kwa upande wa Man United alikuwa ni David de Gea  kwani alizuia vizuri mpira huo.
Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa De Gea kuokoa penalti tangu mwaka 2016 alipofanya hivyo kwenye mchezo dhidi ya Everton na katika penalti iliyopigwa na Romelu Lukaku.
Kipa huyo hakuwahi kudaka penalti yeyote kuanzia mwaka huo hadi sasa ambapo ni jumla ya penalti 40 alizowahi kupigiwa kwenye lango lake.
Mbali ya De Gea kutoa gundu Miongoni mwa stori kubwa katika mchezo huo ilikuwa ni Cristiano Ronaldo aliyeisawazishia  Man United bao dakika ya 35 ikiwa ni dakika tano baada ya West kuongoza kwa bao  ililofunga dakika ya 30 kupitia kwa Said Benrahma.
Ronaldo ameweka rekodi yakuwa mchezaji  pekee kufunga katika viwanja vingi kwenye historia ya ligi tano bora barani Ulaya  ambapo uwanja huo wa London Studium ulikuwa wa 60 kuuchezea na kufunga.
Staa huyo pia anakuwa amefunga kwenye mechi tatu mfululizo tangu arejee Man United mchezo wa kwanza ukiwa dhidi ya Newcastle United ambapo alifunga mabao mawili, wakati United ikiibuka na ushindi wa mabao 4-1, akafunga bao moja kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Young Boys na akamalizika na mchezo wa jana dhidi ya wagonga nyundo wa Jiji la London, West Ham ambayo ilikuwa inafundishwa na kocha wao wa zamani David Moyes aliyeichukua timu mara  baada ya Sir Alex Ferguson kuondoka, lakini alifurushwa kutokana na matokeo mabaya ambayo timu ilikuwa inayapata.
Vile vile bao la Lingaed limemuweka kwenye orodha yakuwa mchezaji wa 47 waliowahi kuifungia West Ham bao wakiwa wanaichezea na baadae wakaifunga wakiwa na timu pinzani.
Ushindi huo umesogeza Man United hadi nafasi ya pili ikiwa imekusanya pointi 13, nyuma ya Liverpool ambayo pia ina alama 13 lakini imekaa kileleni kutokana tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
West Ham iliendelea kusalia kwenye nafasi ya nane kwa alama zake nane ilizokusanya kwenye mechi tano ambazo imeshinda mbili, sare mbili na kufungwa moja.
Shoo nyingine ya kibabe ilikuwa kule The American Express Community Stadium ambapo Brighton iliibuka na ushindi wa mabao 2-1  mbele ya Leicester City.
 


Advertisement