DAZN yaweka Dola 1 bilioni kombe la dunia la klabu

Muktasari:
- Manchester City na Chelsea kutoka England zitashiriki kukamilisha idadi ya timu 32 zitakazochuana kwenye mashindano hayo yatakayofanyika Marekani Juni mwaka huu.
LOS ANGELES, MAREKANI: KUELEKEA mfumo mpya wa uendeshaji wa Kombe la Dunia la Klabu la FIFA, timu shiriki zinaripotiwa kuwa zitakunja pesa za kutosha baada ya ripoti kufichua kwamba zimetengwa zaidi ya Dola 1 bilioni kama pesa ya haki ya matangazo.
Manchester City na Chelsea kutoka England zitashiriki kukamilisha idadi ya timu 32 zitakazochuana kwenye mashindano hayo yatakayofanyika Marekani Juni mwaka huu.
Mashindano haya yaliyofanyiwa maboresho, yatazipa faida kubwa timu shiriki baada ya kampuni ya DAZN kununua haki ya matangazo ya televisheni kwa kutoa Dola 1 bilioni.
Inaelezwa FIFA imepanga kutoa kiasi chote hicho kwa timu shiriki ili kuyapa mashindano hayo hadhi kwa kufanya kila timu itamani kushiriki.
Pamoja pesa ambazo timu shiriki zitapata kwa kushiriki tu na nafasi zitakazoishia, FIFA imepanga kuwepo kwa utaratibu wa kuzipa mkwanja hadi timu maarufu ambazo hazitashiriki.
Ingawa Dola 1 bilioni siyo pesa kubwa sana katika soka ukilinganisha na mashindano mengine kama Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo timu zinagawana Pauni 2 bilioni, upekee wa mkwanja huu ni kwamba unapatikana ndani ya muda mchache kwani timu itakayofika fainali itacheza mechi saba tu wakati Ligi ya Mabingwa ni karibia mechi 13.
Kwenye kombe hili la dunia, kila timu itacheza michezo mitatu tu katika hatua ya makundi kisha hatua nne za mtoano, jumla ya saba.
Barani Ulaya kuna timu 12 zitakazoshiriki ambapo Man City na Chelsea zimefuzu kwa kuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2023 na 2021.
Inaelezwa jumla ya pesa ambazo zimetengwa mezani kwa ajili ya zawadi na uendeshaji wa mashindano haya ni Dola 2 bilioni na zawadi za ushiriki hazitatolewa kwa timu moja kwa moja badala yake zitapelekwa kwa mashirikisho ya mabara ambapo timu shiriki kutoka mabara husika zitalipwa kutoka huko ingawa baadhi ya timu zitakunja pesa nyingi zaidi kuliko nyingine.
Kiujumla katika Dola 1 bilioni, Dola 575 milioni zitatolewa kama sehemu ya ushiriki kisha Dola 465 zitatolewa kwa klabu moja kwa moja kutokana na viwango zitakavyoonyesha katika mashindano.
Mbali ya udhamini wa DAZN ambao umezalisha mkwanja wa kutosha, FIFA pia imeingia mkataba wa udhamini na kampuni ya Coca Cola, Bank of America, kampuni ya elektroniki ya Hisense ya China na AB InBev.
Ikiwa imebakia miezi michache kabla ya kuanza kwa michuano hii, tovuti ya Daily Mail imefichua kuwa bei za tiketi zimepungua.
"Gharama za viti vya bei nafuu kwa mechi katika hatua ya mtoano na kuendelea zimepunguzwa hadi Dola 385. Tiketi za bei nafuu zaidi kwa nusu fainali kwa wale mashabiki wa timu wenyeji zilikuwa zikiuzwa kwa Dola 526 lakini sasa mashabiki wanaweza kuzipata kwa Dola 140.
Na tiketi za bei nafuu zaidi kwa fainali ambazo zilikuwa zikiuzwa kwa Dola 892 sasa zinatolewa kwa bei ndogo ya Dola 300.
FIFA imesisitiza kuwa hatua hii si kupunguzwa kwa bei bali ni katika mpango wao wa kuwashukuru mashabiki waaminifu watakaosafiri hadi Marekani.
Bingwa wa mashindano anakadiriwa anaweza kupata Dola 90 milioni ikiwa inakaribia mara 20 ya ilivyokuwa mashindano yaliyopita ambapo bingwa alipata Dola 5 milioni ambapo timu shiriki zilikuwa ni saba.
Badala ya timu saba, sasa zitakuwa na timu 32 kutoka duniani kote, ikiwa ni pamoja na 12 kutoka Ulaya na mbali ya Man City na Chelsea, timu kubwa kama Bayern Munich, Real Madrid na Paris Saint-Germain pia zitakuwapo.
Mashindano haya yamekumbwa na ukosoaji kutokana na kuongezeka kwa mzigo wa mechi nyingi za kucheza kwa wachezaji.