Dani Alves, mkewe wapata mtoto
Muktasari:
Alves, raia wa Brazil, alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela Februari mwaka jana baada ya jopo la majaji watatu kumpata na hatia ya shambulio la kingono kufuatia kesi iliyochukua siku tatu. Wakati wa kesi hiyo, uhusiano wake na mkewe Sanz, mwanamitindo mwenye umri wa miaka 33 ulidorora sana, na ilidaiwa kuwa walitengana, ingawa haikuwahi kuthibitishwa rasmi kwamba walitalikiana.
RIO DI JANEIRO, BRAZIL: BEKI wa zamani wa Barcelona, Dani Alves, na mkewe Joana Sanz wamebarikiwa kupata mtoto wao wa kwanza pamoja, miezi saba baada ya hukumu yake ya ubakaji kufutwa, kwa mujibu wa ripoti.
Alves, raia wa Brazil, alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela Februari mwaka jana baada ya jopo la majaji watatu kumpata na hatia ya shambulio la kingono kufuatia kesi iliyochukua siku tatu. Wakati wa kesi hiyo, uhusiano wake na mkewe Sanz, mwanamitindo mwenye umri wa miaka 33 ulidorora sana, na ilidaiwa kuwa walitengana, ingawa haikuwahi kuthibitishwa rasmi kwamba walitalikiana.
Mwanzoni, Sanz alimsaidia mumewe, lakini uhusiano wao uliharibika baada ya hukumu kutolewa. Alionekana akichapisha selfie yenye ishara ya ushindi muda mfupi baada ya Alves kuhukumiwa kifungo cha miaka minne na nusu gerezani.
Hata hivyo, baada ya Alves kupewa dhamana, wawili hao walionekana kupatana tena, na Sanz akafichua kuwa walipitia mizunguko miwili ya matibabu ya IVF na kupoteza ujauzito mara tatu kabla ya hatimaye kutangaza ujauzito wake wa kwanza.
Kwa mujibu wa tovuti ya burudani ya Hispania Vanitatis, sasa wamempokea mtoto wa kiume na wamerudi nyumbani baada ya kujifungua.
Jina la mtoto halijatajwa rasmi, ila linadaiwa kuanza na herufi “J”. Sanz alijifungulia mjini Barcelona, kisha akasafiri na mumewe hadi Esplugues de Llobregat.
Sanz aliandika ujumbe wa kugusa moyo kupitia Instagram mapema mwaka huu:
“Sikutaka kushiriki chochote hadi iwe wazi kabisa, lakini nilitaka kushiriki kwa ajili ya wale wanaopambana. Tangu nikiwa na umri wa miaka 22, nimekuwa nikiulizwa, ‘Mtoto atakuja lini?’ Shinikizo la kijamii ni la kutisha.
“Sikuwahi kuwa na hisia za kuwa mama au hamu ya kupata mtoto. Miaka ilivyopita, marafiki zangu walianza kupata watoto na mitandao ya kijamii ikajaa picha za kuzaliwa labda ni hatua ya maisha.
“Maneno kama ‘muda wako unaisha’ si mzaha. Watu hawajui ugumu wa kupata mimba na jinsi umri unavyoathiri. Miaka mitano iliyopita nilikuwa na hofu kubwa ya kuwa mama hofu ya kiumbe kutegemea mimi, hofu ya kupoteza kazi, na hofu ya kupoteza utambulisho wangu kama mwanamke.”
Baada ya hukumu ya awali, waendesha mashtaka wa umma waliwasilisha rufaa wakitaka Alves ahukumiwe miaka tisa, huku waendesha mashtaka binafsi waliokuwa wakimwakilisha mlalamikaji wakitaka ahukumiwe miaka 12.
Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Catalonia ilikataa rufaa zote na kumuachilia huru Alves, ikisema katika uamuzi wake wa kurasa 101 kwamba:
“Haiwezi kuhitimishwa kuwa mipaka ya dhana ya kutokuwa na hatia imevukwa.”
Tangu Machi mwaka jana, Alves alikuwa akiishi kwa dhamana, na baada ya kuachiwa rasmi, kupitia wakili wake Ines Guardiola, amesema kuwa “ana furaha sana”.
Sanz, naye, ameandika ujumbe kwenye Instagram akiashiria faraja baada ya kipindi kigumu:
“Walinielekezea vidole, wakaniita majina, wakanitishia na kunisakama kwa miaka miwili. Kama vile mimi ndiye nilikuwa niliyehukumiwa.
“Licha ya madhara yote ya vyombo vya habari na jamii, bado nimesimama imara, bila kupoteza kazi hata moja kama wengine walivyotamani, nikiendelea kusimamia imani zangu bila kuathiriwa na chuki.
“Naomba watu waache kutoa chuki kwa watu wasio wajua. Elimisheni nafsi zenu kabla ya kuhukumu wengine.”
Kwa sasa, Dani Alves na Joana Sanz wanafurahia maisha mapya kama wazazi, hatua inayokuja baada ya kipindi kigumu cha kisheria na kihisia kilichotikisa maisha yao kwa muda mrefu.