Alves, Robinho wawe darasa tosha kwetu

Muktasari:

  • Huyo ni Alves, beki ambaye aliteka hisia za wengi kutokana na kiwango bora alichokuwa akikionyesha uwanjani pamoja na mataji mengi aliyoshinda lakini mkono wa sheria haukumwonea huruma kutokana na makosa aliyofanya.

SIKU chache zilizopita tumeshuhudia mchezaji wa zamani wa Brazil na Barcelona, Dani Alves akitoka gerezani kwa dhamana ili kusubiria rufaa yake ya kupinga adhabu ya kifungo cha miaka minne na nusu jela, baada ya kukutwa na hatia ya makosa ya ubakaji na udhalilishaji kingono aliyofanya huko Hispania miaka ya nyuma.


Huyo ni Alves, beki ambaye aliteka hisia za wengi kutokana na kiwango bora alichokuwa akikionyesha uwanjani pamoja na mataji mengi aliyoshinda lakini mkono wa sheria haukumwonea huruma kutokana na makosa aliyofanya.


Makosa yake hayakuishia katika kifungo tu bali Barcelona ilimuondoa katika orodha yake ya wachezaji magwiji klabuni hapo huku mikataba yake mingi ya udhamini binafsi ikivunjwa kama njia ya kuonyesha kampuni na taasisi zilizofanya naye kazi haziungi mkono kile alichofanya.


Wakati Alves akitolewa kwa dhamana, mchezaji mwingine nyota wa zamani wa Brazil yeye alikutana na rungu la kutakiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka tisa jela baada ya kukutwa na hatia ya makosa kama yale yaliyofanywa na Alves.


Robinho alifanya na kukutwa na hatia ya makosa hayo akiwa Italia ambako alihukumiwa adhabu hiyo lakini alikimbilia kwao Brazil akiamini angeweza kukwepa kifungo lakini mahakama nchini humo iliamua adhabu aliyopewa Italia ataitumikia nchini mwao kwa vile haiungi mkono makosa ya ubakaji na udhalilishaji kingono.


Kilichotokea kwa Robinho na Alves kinapaswa kuwa fundisho kwa wachezaji wetu hapa nchini kuwa hakuna aliye juu ya sheria na kila mmoja anapaswa kuwa na nidhamu kubwa maisha mwake ili kuepuka kufanya makosa ambayo yatamgharimu.


Wasijione kama kuwa wachezaji kutakuwa kinga kwao pale wanapofanya makosa ya uvunjaji wa sheria za nchi pindi wakiwa nje ya uwanja na badala yake wanapaswa kujitunza na kujilinda ili kuepuka hiki kilichotokea kwa wenzao.


Badala yake wao ndio wanatakiwa kuwa mfano bora kwenye jamii kwa kuepuka mtindo wa maisha ambao unaharibu taswira zao na timu wanazochezea.


Mchezo wa soka unafuatiliwa na kundi kubwa la watu sio tu hapa nchini bali duniani hivyo kile kinachofanywa na wachezaji kinaonekana haraka iwe kibaya au kizuri.