Cristhian Mosquera apewa mchongo Colombia
Muktasari:
- Beki huyo ni nahodha wa timu ya taifa ya Hispania ya chini ya umri wa miaka 21, lakini amekuwa akipewa kisogo na kocha wa timu ya Hispania ya wakubwa, Luis de la Fuente kumjumuisha kwenye kikosi chake. Mosquera alizaliwa Alicante, Hispania na wazazi wa kutoka Colombia.
LONDON, ENGLAND: BEKI wa kati, Cristhian Mosquera huenda akabadilisha soka lake la kimataifa kutoka Hispania hadi Colombia baada ya kufanya vizuri kabisa Ligi Kuu England akiwa na kikosi cha Arsenal
Beki huyo ni nahodha wa timu ya taifa ya Hispania ya chini ya umri wa miaka 21, lakini amekuwa akipewa kisogo na kocha wa timu ya Hispania ya wakubwa, Luis de la Fuente kumjumuisha kwenye kikosi chake. Mosquera alizaliwa Alicante, Hispania na wazazi wa kutoka Colombia.
Anamiliki hati za uraia wa nchi zote mbili, Hispania na Colombia na alijiunga na Arsenal kwa ada ya Pauni 13 milioni dirisha lililopita la majira ya kiangazi mwaka huu.
Tangu wakati huo, amecheza mechi nne kwenye kikosi hicho cha Arsenal msimu huu, huku mechi tatu zilimalizika kwa timu hiyo ya Kocha Mikel Arteta bila kuruhusu bao.
Arteta amefichua kuvutiwa na beki huyo. Alionekana kufanya mazoezi kwenye kikosi cha Hispania, Septemba, lakini bado hajacheza mechi yoyote kwenye kikosi cha wakubwa.
Mashabiki waliamini mechi yake ya kwanza ingekuja baada ya beki wa Real Madrid, Dean Huijsen kulazimika kuondoka kwenye kikosi cha timu ya taifa kilichokuwa kikijiandaa na mechi za kufuzu Kombe la Dunia kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli.
Lakini, badala yake, beki wa kati wa Athletic Bilbao, Aymeric Laporte, ndiye aliyeitwa kuja kuchukua nafasi ya beki Huijsen. Na sasa, Colombia imempa nafasi beki huyo kwenda kupata fursa ya kucheza kikosi cha wakubwa baada ya kushindwa kumshawishi mwaka 2023.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kwenda kuichezea Colombia, amesema: “Kitu ambacho kipo kwangu ni kupambana siku hadi siku na milango itafunguka.”
Shirikisho la soka la Hispania linaamini Mosquera ataendelea kuitumikia Hispania kwenye soka la kimataifa na wanaamini atakuwa na nafasi kubwa ya kuitumikia La Roja.