Conte, Napoli wakati wowote mazingira yatabadilika
Muktasari:
- Kocha huyo Mtaliano ameibua wasiwasi zaidi baada ya kutangazwa kwamba hatakuwapo kwenye mazoezi ya kikosi cha Napoli hadi Jumatatu ijayo.
NAPLES, ITALIA: KIBARUA cha kocha Antonio Conte huko Napoli kipo kwenye hali ya sintofahamu kutokana na kile kilichotokea wikiendi iliyopita.
Kocha huyo Mtaliano ameibua wasiwasi zaidi baada ya kutangazwa kwamba hatakuwapo kwenye mazoezi ya kikosi cha Napoli hadi Jumatatu ijayo.
Msaidizi wa muda mrefu wa Conte, Cristian Stellini, ambaye aliwahi kuwa kocha wa mpito Tottenham wakati bosi wake alipoachana na timu hiyo, ndiye atakayesimamia mazoezi ya Napoli.
Kuthibitisha hilo, Napoli iliandika: “Bwana Antonio Conte, kama ilivyopangwa na kukubaliana na klabu, atarejea kwenye viwanja vya mazoezi vya Napoli, Jumatatu, Novemba 17.”
Conte aliongoza Napoli kunyakua taji la Serie A msimu uliopita, huku akipata huduma bora kabisa kutoka kwa mastaa kama Scott McTominay na Romelu Lukaku walipoisaidia timu hiyo kuibwaga Inter Milan kwenye ubingwa.
Lakini, msimu huu, mambo yameenda kombo kwa Conte. Baada ya kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Bologna, Jumamosi iliyopita, Conte alibwata: “Lazima tufanye kitu. Sitaki kuambatana na mfu, hili lazima lifahamike wazi. Kama tunataka kufanya kitu pamoja, sawa, sivyo sote tunapaswa kuwajibika.”
“Hicho ndicho kitu ninachofanya mara zote.”
Kwenye kubwata kwake, Conte alimweka kando Rasmus Hojlund kwenye ukosoaji wake, amesema: “Sina shida na Hojlund, bila shaka alikuwa mchezaji bora wa uwanjani. Alishambulia kwa nguvu zake zote, kama kiwango chake kinajadiliwa kwenye mabao, ni sawa. Tunapaswa kuandaa mambo machache, tunapaswa kumsapoti.”
Licha ya Conte kubwata, Napoli ipo nyuma kwa pointi mbili tu kufikia kelele cha Serie A.
Na rais wa klabu ya Napoli, Aurelio de Laurentiis, naye alipuuzia madai kwamba kocha wa timu hiyo ataondoka, aliposema: “Nimekutana na hii kitu ya Conte kujiuzulu. Siku zote nimekuwa nikiheshimiana na Conte. Kwa mashabiki waliosikia hizo taarifa zisizokuwa na maana, ninasema: najivunia kuwa na mwanaume wa kweli kama Antonio Conte. Nimejitoa mhanga kwa kila sekunde na amekuwa mtu wa kujitoa. Hiki ndicho kitu tulichojihakikishia kutoka kwake kwenye klabu na kuwa kitu kinachohitajika kwenye klabu kama hii aina ya Napoli.”