Napoli yashindwa kufunga tena ikitoka suluhu na Frankfurt
Muktasari:
- Kikosi cha Antonio Conte kilikuwa kinatafuta kujirekebisha baada ya kichapo cha mabao 6–2 kutoka kwa PSV Eindhoven katika mchezo wa tatu wa makundi, lakini kilihangaika kutengeneza nafasi huku kikimkosa kiungo Kevin De Bruyne aliye majeruhi.
NAPLES, ITALIA: NAPOLI imeshindwa kufunga kwa mara ya pili mfululizo baada ya mabingwa hao wa Italia kulazimishwa matokeo ya suluhu nyumbani dhidi ya Eintracht Frankfurt kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mechi ikichezwa Stadio Diego Armando Maradona, leo Jumanne Novemba 4, 2025.
Kikosi cha Antonio Conte kilikuwa kinatafuta kujirekebisha baada ya kichapo cha mabao 6–2 kutoka kwa PSV Eindhoven katika mchezo wa tatu wa makundi, lakini kilihangaika kutengeneza nafasi huku kikimkosa kiungo Kevin De Bruyne aliye majeruhi.
Napoli ilianza vizuri lakini ikakosa mawasiliano katika eneo la mwisho la uwanja. Rasmus Hojlund na Frank Anguissa waligongana wakijaribu kuunganisha krosi ya Eljif Elmas, kabla ya winga huyo kuona shuti lake lililoelekea wavuni likiokolewa kimakosa na Scott McTominay.
Kiungo huyo wa Scotland alipoteza nafasi mbili za wazi katika kipindi cha pili, kwanza aliposhindwa kumalizia baada ya kumpiga chenga kipa wa Frankfurt, Michael Zetterer, kisha baadaye akapiga juu ya lango baada ya kupokea pasi ya Anguissa.
Mchezaji wa akiba wa Frankfurt, Ansgar Knauff, alimlazimisha kipa wa Napoli, Vanja Milinkovic-Savic, kuokoa hatari kwa shuti la karibu, lakini timu hiyo ya Bundesliga pia ilionekana kukosa ubora katika safu ya ushambuliaji.
Zetterer aliokoa mara mbili katika dakika za majeruhi na kuhakikisha Napoli inapata sare nyingine tasa nyumbani, baada ya kutoka 0–0 na Como kwenye Serie A, Jumamosi iliyopita.
Katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, Napoli na Frankfurt sasa zina pointi nne kila moja baada ya kushuka dimbani mara nne.