Antonio Conte achimba mkwara Napoli
Muktasari:
- Bologna ilipata ushindi wa kushawishi wa 2-0 dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Serie A, shukrani kwa mabao ya Jhon Lucumi na Thijs Dallinga.
NAPLES, ITALIA: KOCHA, Antonio Conte ameripotiwa kuibua shaka kubwa kuhusu hatima yake kwenye kikosi cha Napoli baada ya kuwa mbogo kufuatia kichapo cha kutoka kwa Bologna kwenye mchezo wa Serie A uliofanyika Jumapili iliyopita.
Bologna ilipata ushindi wa kushawishi wa 2-0 dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Serie A, shukrani kwa mabao ya Jhon Lucumi na Thijs Dallinga.
Hicho kilikuwa kichapo cha tano kwa Napoli katika michuano yote msimu huu na ilikuwa mechi ya tatu mfululizo kwa kikosi hicho cha Conte kushindwa kufunga bao.
Baada ya mechi, Conte amesema: “Kama unapoteza mechi tano, hiyo ina maana kuna kitu hakipo sawa. Kuna kitu lazima kifanyike, kwa sababu sitaki kuambatana na wafu. Mimi nitakuwa mtu wa kwanza kuwajibika. Naona kabisa kuna mpasuko na nitazungumza na klabu juu ya hilo.
“Sioni ile hamasa, lakini kila mtu anafikiria matatizo yake. Hakuna tiba ya upandikizaji wa moyo. Kila mmoja wetu ni lazima ajitafute. Kuna vitu lazima vifanyike, lakini tujue tunavifanyaje.
“Hicho ni moja ya vitu vya kufanyika kazi na kama timu lazima tuwe na matarajio makubwa. Kila mtu afikirie kwenye eneo lake na nitakwenda kuzungumza na mabosi kuhusu hili.”
Kinachoelezwa ni kwamba Conte amepanga kwenda kufanya mazungumzo mazito na mabosi wa klabu hiyo ili kutambua kwa ufasaha juu ya mipango ya timu baada ya kuona mambo yamezidi kwenda kombo kwenye kikosi hicho cha Italia ikiwamo kwenye Serie A na Ligi ya Mabingwa Ulaya.