Conte macho kodo kwa straika Zirkzee
Muktasari:
- Hilo linakuja baada ya kocha huyo kukoshwa na kiwango cha kiungo Scott McTominay, ambaye alimsajili kutoka Man United kwa ada ya Pauni 25 milioni kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
NAPLES, ITALIA: KOCHA wa Napoli, Antonio Conte anapiga mpango wa kuvamia tena Manchester United kujaribu kumsajili staa wa timu hiyo kwenye dirisha la Januari.
Hilo linakuja baada ya kocha huyo kukoshwa na kiwango cha kiungo Scott McTominay, ambaye alimsajili kutoka Man United kwa ada ya Pauni 25 milioni kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
Kwa mujibu wa Il Mattino, Conte, 55, sasa anampigia hesabu mchezaji Joshua Zirkzee, ambaye amekuwa akipambana na hali yake akijitafuta tangu alipojiunga na Man United kwenye dirisha lililopita.
Man United ilimsajili Zirkzee, 23, kutoka Bologna kwa ada ya Pauni 36.5 milioni. Hata hivyo, tayari imekuwa ikivumishwa kwamba straika huyo anapiga hesabu za kuachana na timu hiyo, huku Juventus ikifuatilia kwa karibu uwezekano wa kumsajili.
Na sasa, Napoli nayo inahitaji saini ya staa huyo wa kimataifa wa Uholanzi.
Kinachoripotiwa ni kwamba Conte amepewa ruhusa ya kuingia kwenye mbio za kuhitaji saini ya fowadi huyo. Zirkzee huenda akashawishika na mpango wa kurudi kukipiga Serie A, mahali ambako alipata mafanikio msimu uliopita, alifunga mabao 12 na asisti saba katika mechi 37.
Conte ni shabiki mkubwa wa mshambuliaji huyo na alitaka kumsajili kwenye dirisha lililopita kabla ya kuzidiwa kete na Man United. Kwenye kikosi hicho cha Old Trafford, Zirkzee amefunga mabao matatu na kuasisti mawili katika mechi 21.