Conor Mcgregor atiwa hatiani, UFC yamfungia miezi 18
Muktasari:
- McGregor alishindwa kutoa ushirikiano kwenye idara ya kupambana na kuzuia dawa za kusisimua misuli ‘Combat Sports Anti-Doping (CSAD)’ ambayo hufanya vipimo kwa niaba ya UFC.
Conor McGregor amekubali adhabu ya kufungiwa kwa miezi 18 kushiriki katika mashindano ya Shirikisho la Mchezo wa Ngumi na Mateke (UFC) baada ya kukiuka sheria ya kupambana na dawa za kulevya ya shirikisho hilo.
McGregor alishindwa kutoa ushirikiano kwenye idara ya kupambana na kuzuia dawa za kusisimua misuli ‘Combat Sports Anti-Doping (CSAD)’ ambayo hufanya vipimo kwa niaba ya UFC.
Bondia huyo alishindwa kufanya hivyo mara tatu, hali ambayo imepelekea kuchukuliwa kama kosa chini ya sera ya kupambana na dawa za kusisimua misuli ya UFC. Alitakiwa kufanya vipimo Juni 13, 2024, Septemba 19, 2024 na Septemba 20, 2024.
Kwa sababu hiyo, McGregor amekubali kutoshiriki mashindano ya UFC kwa kipindi cha miezi 18, ambacho kitaanza kuhesabiwa kuanzia Septemba 20, 2024 siku aliyokosa jaribio la tatu. Hii ina maana ataruhusiwa kurudi kupigana kuanzia Machi 20, 2026, wakati ambao UFC inapanga kuwa na tukio maalum katika Ikulu ya Marekani (White House) Juni 14, 2026.
Wapiganaji wote wa UFC wanatakiwa kutoa taarifa sahihi za mahali walipo wakati wote ili waweze kupimwa bila taarifa ya awali. Kwa hiyo, McGregor amethibitika kuwa na makosa ya kushindwa kutoa ushirikiano na kusema mahali alitakiwa kufanyiwa vipimo hivyo chini ya CSAD.
McGregor hajapigana tangu Julai, 2021 alipovunjika mguu katika pambano lake la tatu dhidi ya Dustin Poirier. Aliratibiwa kurudi kupigana dhidi ya Michael Chandler Juni 29, 2024 lakini akajiondoa Juni 13, 2024 kwa sababu ya kuvunjika kidole cha mguu.
CSAD ilibaini kuwa wakati wa vipimo hivyo alivyokosa, McGregor alikuwa akiuguza majeraha na hakuwa katika maandalizi ya pambano lolote.
McGregor ameripotiwa kushirikiana kikamilifu baada ya kutuhumiwa na CSAD kwa kukubali makosa yake, na kutoa maelezo ya kina yaliyosaidia kufafanua sababu za kukosa vipimo hivyo. Kwa sababu ya ushirikiano wake, marufuku hiyo imepunguzwa kutoka miezi 24 hadi miezi 18.
Hii ni mara ya kwanza kwa McGregor kukumbwa na kosa la kukiuka sera ya kupambana na dawa za kusisimua misuli ya UFC.
Hata huivyo hadi sasa hajatoa tamko lolote rasmi kuhusu uamuzi huo.
Tukio hili linakuja muda mfupi baada ya bingwa huyo wa zamani wa UFC kutangaza kuanza mapumziko kutoka kwenye mitandao ya kijamii na kujiondoa katika kinyang’anyiro cha urais wa Ireland.
Ameandika: “Hey watu wa mtandaoni, nipo nje kwa muda kidogo, tutaonana tena karibuni! Upendo wangu haubadiliki! Asanteni nyote.”
McGregor ambaye sasa amerudi mazoezini kwa ajili ya mipango ya kupigana katika tukio la White House amekuwa akigubikwa na utata tangu aweke silaha chini.
Desemba 2024, alikutwa na hatia katika kesi ya madai ya shambulio la kingono dhidi ya Nikita Hand, tukio lililotokea mwaka 2018 katika hoteli ya kifahari ya Beacon huko Dublin. Alilazimika kumlipa Hand pauni 206,000 kama fidia pamoja na gharama za kisheria baada ya kushindwa kwenye rufaa ya kesi hiyo.
Mnamo Machi 2025, alidokeza kuwa angeweza kustaafu wakati wa mkutano na wanahabari wa Bare Knuckle kabla ya kutengua kauli yake.
Julai 2025, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza mipango ya kuandaa pambano la UFC katika bustani ya Ikulu ya Marekani (White House), litakalofanyika tarehe ya kuzaliwa kwake Juni 14, 2026, ambapo atakuwa anafikisha miaka 80.
Rais wa UFC, Dana White, anafanya mazungumzo ya kuhakikisha tukio hilo linafanyika na kumrudisha McGregor kwenye ulingo. Tukio hilo litahudhuriwa na watu takribani 5,000 chini ya ulinzi mkali.