CHRIS PAUL: Sio nguvu tu, hata mkwanja upo

Muktasari:
- Paul mwenye umri wa miaka 39, amekuwa katika kiwango bora kwa msimu huu na kasi yake ndio inaonekana kushangaza watu wengi kwani licha ya umri wake ameendelea kuwa katika kiwango kilekile.
WINSTON-SALEM, MAREKANI: MIONGONI mwa wachezaji wa NBA ambao hawajakosa kucheza mechi hata moja msimu huu ni Chris Paul wa New Orleans Pelicans ambaye umri umeshaanza kumtupa mkono.
Paul mwenye umri wa miaka 39, amekuwa katika kiwango bora kwa msimu huu na kasi yake ndio inaonekana kushangaza watu wengi kwani licha ya umri wake ameendelea kuwa katika kiwango kilekile.
Mbali ya maajabu anayoyaonyesha kiwanjani, mfukoni pia Paul yupo vizuri akiwa mmoja kati ya wachezaji wa kikapu wenye mkwanja wa kutosha kutokana na mshahara wake na biashara zake za nje ya uwanja. Hapa tumekusogezea.

ANAPIGAJE PESA
Kwa mujibu wa jarida la Forbes, jamaa anashika namba 31 kwa kuwa mwanamichezo mwenye mkwanja mrefu zaidi duniani hadi kufikia mwaka 2021, lakini alishika nafasi ya pili kwenye msimu uliopita wa NBA kwa kuwa mchezaji aliyevuna pesa nyingi zaidi akikunja Dola 40 milioni.
Mbali ya mshahara ambao kwa mwaka huvuka zaidi ya Dola 40 milioni, Paul anavuta mkwanja mwingine kupitia madili yake nje ya uwanja ambapo kwa ujumla anapata Dola 8 milioni kutokana na ubalozi wake wa kampuni za Nike, Air Jordan, Panini, Tissot na State Farm.
Mbali ya ubalozi wake wa kampuni mbalimbali, kuna mkwanja mwingine anaupata kupitia uwekezaji mkubwa alioufanya kwa kampuni kama Hyperice ambako amewekeza zaidi ya Dola 48 milioni, pia ana hisa katika biashara nyingine kama Chirpify RSPCT Basketball na Beyond Meat. Kijumla anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 180 milioni.

MIJENGO
Ana nyumba mbili, ya kwanza ni ile yenye thamani ya Dola 11.1 milioni iliyopo huko Encino, California Marekani.
Hapa amejenga nyumba mbili sehemu moja ambazo zipo ndani ya uzio mmoja, hivyo nyumba moja anaitumia kwa ajili ya wageni na nyingine ni kwa ajili yake na familia yake mwenyewe.
Nyumba zote zimepambwa na vivutio kibao ndani yake ikiwa ni pamoja na mabwawa ya kuogelea na viwanja vya kuchezea michezo mbalimbali.
Mjengo mwingine alikuwa nao huko Woodland Hills, Los Angels lakini aliuuza kwa Dola 1.95 milioni wakati anahama jijini humo.

MAGARI
Jamaa ana ndinga kibao ikiwa ni pamoja na Jeep JKU Wrangler Unlimited, Range Rover na 1977 Chevrolet Monte Carlo.
kijumla magari yake yote yanakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 4 milioni.

MSAADA KWA JAMII
Mara kadhaa ameonekana katika shughuli nyingi za kuchangia jamii na kati ya hizo ni kampeni ya After-School All-Stars ambayo ina lengo la kutoa msaada wa kipesa kwa wanafunzi wasio na uwezo wa kulipa ada.
Vilevile amewahi kushiriki mara kadhaa kwenye kampeni kama Aid Still Required, Boys & Girls Clubs of America, Girl na Make It Right.
Mbali ya yote anamiliki taasisi yake mwenyewe iitwayo CP3 Foundation ambayo amekuwa akiitumia kusaidia watu wasiojiweza.

MAISHA NA BATA
Yupo kwenye ndoa na mrembo Jada Crawley ambaye amezaa naye watoto wawili, mmoja ni wa kike na mwingine ni wa kiume. Alifunga ndoa mwaka 2011.