Chopa ya Neymar yazuiliwa Brazil

SANTOS,BRAZI: Supastaa Neymar ameshindwa kusafiri na helikopta yake yenye thamani ya Pauni 10 milioni baada ya kuzuiwa na mamlaka za anga Brazil.


Kinachoelezwa, kibali kinachoruhusu chopa hiyo kufanya safari zake kimekwisha muda wake. Na sasa, Neymar hataweza kutumia usafiri wake huo hadi hapo atakapopata kibali kingine na kwa kawaida kibali chenyewe hufika mwisho kila baada ya miaka mitatu.


Helikopta hiyo ilikuwa imehifadhiwa Brazil, lakini Neymar alikuwa akiitumia huko Paris wakati alipokuwa akiichezea Paris Saint-Germain.


Helikopta hiyo imegharimu Pauni 10 milioni na ilinunuliwa na kampuni ya Neymar mwaka 2019. Supastaa huyo, huko nyuma alikuwa akimiliki helikopta nyingine mbili ikiwamo Cessna C yenye uwezo wa kubeba abiria 12.


Neymar anaripotiwa kuwa na pato kiasi cha Pauni 250 milioni na amekuwa akipatiwa zawadi ya vitu vya thamani kubwa huko Saudi Arabia baada ya kujiunga na klabu ya Al-Hilal kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.


Sambamba na mkataba wa kulipwa Pauni 2.5 milioni kwa wili, Neymar amepewa pia magari manane ya kifahari ikiwamo Bentley Continental GP, Aston Martin DBX na Lamborghini Huracan. Amepewa pia nyumba na wafanyakazi watatu, wakiwamo wapishi na wafanya usafi. Siku za mapumziko, Neymar anaruhusiwa kutembelea kwenye hoteli na migahawa inayomilikiwa na wamiliki wa klabu ya Al Hilal.