Chelsea yapata dawa ya kadi nyekundu
Muktasari:
- Chelsea tayari imepata kadi nyekundu tatu katika michezo ya ligi Kuu msimu huu na jumla ya kadi tano kwenye mashindano yote ikiwa ni pamoja na kadi moja aliyopewa kocha Maresca mwenyewe.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya hali ya kuonyeshwa kwa kadi nyekundu kwa wachezaji wa Chelsea kukithiri, kocha wa timu hiyo, Enzo Maresca amefichua wachezaji wa klabu hiyo wameweka utaratibu wa kujitoza faini wao kwa wao kama njia ya kudhibiti tatizo hilo linalozidi kuwa kubwa.
Chelsea tayari imepata kadi nyekundu tatu katika michezo ya ligi Kuu msimu huu na jumla ya kadi tano kwenye mashindano yote ikiwa ni pamoja na kadi moja aliyopewa kocha Maresca mwenyewe.
Hii ni nusu ya rekodi yao ya Ligi Kuu msimu wa 2007/08 na ilipata kadi nyekundu sita ikiwa ni jumla ya kadi nane katika mashindano yote.
Ikiwa kasi hiyo itaendelea, Chelsea inaweza kumaliza msimu huu ikiwa na wachezaji 14 waliotolewa nje kwa kadi nyekundu na itavunja rekodi ya sasa ya kadi tisa iliyowekwa na Sunderland msimu wa 2009/10 na Queens Park Rangers, 2011/12.
Maresca amekiri hilo ni tatizo kubwa, ambalo pia limeathiri matokeo ya timu yake ambayo ilipoteza mechi mbili za ligi baada ya kuwa pungufu.
Hata hivyo, wachezaji wameamua kuchukua hatua wenyewe, kwa kuweka utaratibu wa ndani wa kupigana faini ikiwa mmoja wao atafanya kosa la kinidhamu.
Akizungumza kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Ajax, Maresca mwenye umri wa miaka 45, amesema hana tabia ya kuwaadhibu wachezaji moja kwa moja:
"Nina watoto wanne na wanapofanya kosa, siwapigi wala kuwakemea na badala yake, ninajaribu kuwafundisha ili wasirudie. Ndivyo ninavyopenda kufanya hata kwa wachezaji wangu,” amesema Maresca.
"Kadi nyekundu ya Malo Gusto dhidi ya Nottingham Forest ingeepukika. Kadi ya Joao Pedro pia ingeepukika. Zote kwa kweli zingeweza kuzuilika. Lakini ukiangalia kadi ya Trevoh Chalobah ilikuwa kwa ajili ya timu. Gusto ndio alifanya kosa kubwa. Mechi ilikuwa inakwenda kumalizika, tulikuwa tunaongoza 3-0. Wachezaji walikuwa wakihimizana kutoruhusu bao lakini uamuzi wake ulikuwa mbaya. Ni wazi timu inapopata kadi nyekundu tano au sita, kuna kitu kinahitaji kuboreshwa. Ni jambo ambalo tunalifanyia kazi.
Wachezaji wenyewe wamejiwekea mfumo wao ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo wa kupigana faini pale mmoja wao anapofanya kosa la kinidhamu, huo ni utaratibu wao ambao kimsingi nakubaliana nao."
Katika mechi ijayo, Chelsea itakuwa nyumbani kuvaana na Sunderland katika Ligi Kuu England, mechi ambayo itaanza saa 11:00 jioni, Jumamosi.