Chelsea yaipiga bao Man United kwa Liam Delap

Muktasari:
- Mei 14, tovuti ya The Sun ilifichua kwamba Manchester United iliyokuwa inapewa nafasi kubwa kumpata Delap huenda ikapinduliwa na Chelsea ambayo inaonekana kuwa ndio ndoto ya mchezaji huyo.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA inadaiwa kushinda vita ya kuwania saini ya mshambuliaji wa Ipswich, Liam Delap na huenda ikamtangaza wiki ijayo.
Mei 14, tovuti ya The Sun ilifichua kwamba Manchester United iliyokuwa inapewa nafasi kubwa kumpata Delap huenda ikapinduliwa na Chelsea ambayo inaonekana kuwa ndio ndoto ya mchezaji huyo.
Katika msimu uliopita, Delap mwenye umri wa miaka 22, alifunga mabao 12 licha ya kushuka daraja na Ipswich Town.
Katika mkataba wake ana kifungu kinachomwezesha kuondoka ikiwa timu inayomhitaji italipa Pauni 30 milioni kama ada ya uhamisho. Manchester United walionyesha nia lakini kukosa kushiriki michuano ya Ulaya msimu ujao kumesababisha Delap kuachana nao.
Everton pia walikuwa wanapigania saini ya staa huyu lakini Delap anaonekana kuwa tayari kujiunga na Chelsea kuliko timu yoyote.
Chelsea inaonekana kuwa haitokuwa na shida ya kulipa ada ya uhamisho ianyohitajika kwani inatarajiwa kukunja mpunga wa kutosha kupitia michuano ya Klabu Bingwa Dunia pamoja na kushiriki Ligi ya Mabingwa.
Hata hivyo, mbali ya ada ya uhamisho Ipswich wameomba kupewa kwa mkopo mshambuliaji wa Chelsea, Marc Guiu kama sehemu ya makubaliano ya dili hilo.
Kocha wa Ipswich, Kieran McKenna, alifichua wiki iliyopita kuwa Delap alikuwa anaangalia timu gani atajiunga nayo baada ya Ipswich kushuka. “Liam anaangalia wapi atacheza msimu ujao, jambo ambalo naamini ana haki ya kufanya na tunamuunga mkono. Nadhani tumempa idhini ya kufanya hivyo wiki hii. Ni uamuzi muhimu sana kwa maisha yake ya baadaye. Bila shaka ana hamu kubwa ya kupiga hatua na ana haki ya kufanya hivyo.”