Chelsea yaipa urahisi Arsenal kwa Osimhen
Muktasari:
- Inaelezwa Chelsea imejiondoa katika dili hilo baada ya Napoli kutowapa jibu linaloeleweka juu ya ombi lao la kutaka kupunguziwa bei.
BAADA ya Chelsea kuripotiwa kuachana na mpango wa kumsajili straika wa Napoli, Victor Osimhen katika dirisha hili, ripoti zinadai Arsenal bado inafanya mawasiliano juu ya staa huyo.
Inaelezwa Chelsea imejiondoa katika dili hilo baada ya Napoli kutowapa jibu linaloeleweka juu ya ombi lao la kutaka kupunguziwa bei.
Osimhen ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2026, kwa sasa yupo sokoni lakini timu inayomhitaji itatakiwa kulipa Pauni 111 milioni ili kuuvunja mkataba wake.
Kiasi hicho kimeonekana ni kikubwa kwa Chelsea ambayo tayari imeshafanya usajili wa mastaa kadhaa na ili kuepuka matatizo ya kunyang’anywa pointi kwa kukiuka sheria za matumizi ya fedha, inadaiwa kujiondoa kwenye dili hilo.
Arsenal ambayo hivi karibuni kocha wake Mikel Arteta alisema hawatavunja tena rekodi ya usajili kwa kutoa pesa nyingi kumnunua mchezaji mmoja, taarifa za ndani zinadai inaweza kufanya hivyo ikiwa itafanikisha kuwauza mastaa wanne kati ya saba iliopanga kuwauza katika dirisha hili.
BRIGHTON imefanya mawasiliano na wawakilishi wa beki wa zamani wa Bayern Munich na Borussia Dortmund, Mats Hummels, 35, ili kumsajili katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Beki huyu wa zamani wa Ujerumani huduma yake pia inahitajika na West Ham.
Msimu uliopita alicheza mechi 40 za michuano yote na kufunga mabao matano.
MANCHESTER United imeonyesha nia ya kutaka kumsajili kiungo wa AS Monaco na Ufaransa, Youssouf Fofana, 25, ambaye anahusishwa pia na AC Milan.
Fofana ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwakani, msimu uliopita alicheza mechi 35 za michuano yote na kufunga mabao manne.
KOCHA wa Manchester United bado hajaondoa uwezekano wa kuruhusu kusainishwa mkataba wa kudumu kwa kiungo wa Fiorentina na Morocco, Sofyan Amrabat, 27, aliyecheza kwa mkopo katika timu yao kwa msimu uliopita.
Amrabat ambaye haonekani kuwa tayari kurudi tena Fiorentina kwa msimu ujao, mkataba wake na timu hiyo unamalizika mwakani.
LICHA ya kupendekezwa na benchi la ufundi la Tottenham, usajili wa mshambuliaji wa Bournemouth, Dominic Solanke kutua timu hiyo utategemea na hatma ya Richarlison katika timu hiyo. Richarlison mwenye umri wa miaka 27, anahusishwa kuwa katika rada za timu mbalimbali za Saudi Arabia ambazo huenda zikamsajili katika dirisha hili. Mkataba wa Solanke unamalizika mwaka 2027.
BARCELONA imefikia makubaliano ya awali na RB Leipzig kwa ajili ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Dani Olmo katika dirisha hili.
Staa huyu wa kimataifa wa Hispania aliyeonyesha kiwango bora katika michuano ya Euro mwaka huu kule Ujerumani, anaweza akatua Barca kwa kiasi kinachofikia Pauni 47.3 milioni.
ATLETICO Madrid inataka kuhakikisha inamuuza mshambuliaji Samu Omorodion katika dirisha hili ili kupata pesa itakazotumia kufanya usajili wa Julian Alvarez ambaye tayari imeshafanya makubaliano na Manchester City juu ya kumnunua. Omorodion anawindwa sana na Chelsea ambayo hivi karibuni iliripotiwa kuwa katika mazungumzo na Atletico kuhusu ada ya uhamisho baada ya maafikiano binafsi.
MAZUNGUMZO baina ya vigogo wa Bayern Munich na Bayer Leverkusen juu ya beki Jonathan Tah hadi sasa bado yanaendelea na bado timu pande zote mbili hazijafikia mwafaka. Tah, 28, mkataba wake na Leverkusen unaisha mwakani. Ameivutia Bayern kutokana na kiwango bora alichoonyesha msimu uliopita akiisaidia timu yake kuchukua ubingwa wa Bundesliga.