Chelsea kuchomoa kipa Liverpool

Muktasari:
- Tofauti na dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, Chelsea walikuwa kimya sana katika dirisha la uhamisho lililopita, wakijikita katika kuondoa wachezaji badala ya kusajili.
LONDON, ENGLAND: INAELEZWA kwamba Chelsea wamepanga kufanya uhamisho mkubwa kwa kipa wa Liverpool ambaye tayari amekiri kwamba anataka kuondoka kwenye timu hiyo.
Tofauti na dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, Chelsea walikuwa kimya sana katika dirisha la uhamisho lililopita, wakijikita katika kuondoa wachezaji badala ya kusajili.
Miongoni mwa mastaa walioondoka katika dirisha hilo ni kama Ben Chilwell, Joao Felix, na Axel Disasi waliotolewa kwa mikopo.
Lakini sasa, inaonekana kuwa kocha wao Enzo Maresca anajiandaa kufanya mabadiliko makubwa katika dirisha la uhamisho la majira ya joto ya 2025, kwani ripoti mpya imesema kwamba amemkazia macho kipa wa Liverpool Caoimhin Kelleher.
Alhamisi usiku, Liverpool ilitinga fainali ya Kombe la Carabao baada ya kushinda 4-0 katika mechi yao ya pili ya nusu fainali dhidi ya Tottenham Hotspur, na kuufanya matokeo ya jumla kuwa 4-1 kwa mechi zote mbili.
Mmoja kati ya mihimili muhimu ya Liverpool katika mashindano haya ni Kelleher, ambaye ameanza katika mechi zote.
Licha ya kuwa kipa wa kuaminika kwa Liverpool kwa miaka ya hivi karibuni, inaelezwa staa huyu wa Ireland ataondoka Anfield msimu huu baada ya timu hiyo kuamua kumchukua kipa kutoka Georgia Giorgi Mamardashvili mwaka jana.
Mamardashvili ambaye atarejea Liverpool katika dirisha lijalo akitokea Sevilla anakocheza kwa mkopo, atasababisha Kelleher kuondoka kwa sababu anaona atapata nafasi finyu zaidi ya kucheza.
Maresca ameamua kutafuta kipa mwingine kwa sababu haridhishwi na viwango vya Robert Sanchez na Filip Jorgensen ambao ndio anawatumia kwa sasa.
Kelleher amewahi kukiri awali kwamba yupo tayari kuondoka Liverpool ili kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akiichezea Ireland mwezi Septemba, Kelleher alisema: "Nimekuwa wazi katika miaka michache iliyopita kwamba nataka kwenda mahali na kuwa namba moja. Klabu imefanya uamuzi wa kumchukua kipa (Mamardashvili), jambo ambalo linaonekana kama wamechukua mwelekeo mwingine. Liverpool wamekataa baadhi ya ofa pia, hivyo sio kila wakati ni mimi ndio ninayeamua kuondoka au kubaki. Lengo langu lipo wazi. Mimi ni mzuri vya kutosha na nataka kwenda kucheza kila wiki."