Chelsea hebu msikieni Wenger

LONDON, ENGLAND

KOCHA Arsene Wenger anaamini Chelsea hawatakuwamo kwenye Top Four ya Ligi Kuu England msimu huu na kwamba msimu wao watamaliza na pointi 63.

Gwiji huyo wa klabu ya Arsenal alizungumzia pointi 43 za sasa za The Blues na kusema kwamba kikosi hicho kinachonolewa na Mjerumani, Thomas Tuchel hakitakuwa na uwezo wa kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Wapinzani wa Chelsea huko London, West Ham United wapo kwenye kiwango bora na na ndio wanaoshikilia nafasi ya nne kwa sasa, pointi tatu juu ya The Blues huku timu zote zikiwa zimecheza mechi 25.

Leicester City na Manchester United zipo pointi nne juu ya West Ham huku wengi wakiamini kwamba huo ni mlima mrefu kwelikweli kwa miamba hiyo ya Stamford Bridge kuweza kuupanda.

Lakini, Wenger haamini kabisa kama Chelsea watakuwa na uwezo wa kumaliza ligi kwenye nafasi nne za juu baada ya sare yao ya 1-1 dhidi ya Southampton Jumamosi iliyopita na alisema: “Naweza kusema ni matokeo mazuri yanayomfanya mtu mmoja afurahi zaidi ya mwingine.

“Southampton watakuwa wamefurahi baada ya kuzuia kupoteza tena. Wasiwasi upo kwa Chelsea kwa sababu hawakuwa kwenye kiwango chao bora na hilo linatokea mara kadhaa kwenye ligi.

“Natazama pointi zao walizonazo kwa sasa, kwa mwendo huo watapata pointi 63. Idadi hiyo haitatosha kuingia kwenye Top Four. Hebu fikiria, pointi 43 kwenye mechi 25 kwa wastani huo, watapata pointi 63 mwisho wa msimu na idadi hiyo, hakika itakuweka nje ya Top Four.” Kocha Tuchel alikosolewa kwenye mechi hiyo ya St Mary’s kwa uamuzi wake wa kumtoa Callum Hudson-Odoi, aliyeingia kwenye kipindi cha pili na kumwingiza Hakim Ziyech kwenye dakika 76.

Wenger amemtetea Tuchel na kusema: “Nimefanya hivyo mara moja kwenye maisha yangu nilikuwa nahofia kupoteza mechi kwa sababu mchezaji alikuwa amepoteza kabisa uwanjani.”