Klopp acheza anga mbaya

Klopp ahofia kikosi kipana cha Chelsea kwa ubingwa

LIVERPOOL, ENGLAND

MAMBO si mambo. Hakika siku zinakwenda kasi sana. Liverpool iliiteka dunia ya soka miezi nane tu iliyopita kutokana na soka la kibabe ililokuwa ikipiga uwanjani. Si siku nyingi zimepita, Julai mwaka jana tu hapo, miamba hiyo ya Anfield ilinyakua taji la Ligi Kuu England, kwa mara ya kwanza kwenye historia yao baada ya kusubiri kwa miaka 30.

Taji hilo lilikuja baada ya kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Klabu Bingwa ya Dunia.

Baada ya kufanikiwa kubeba taji la ligi msimu uliopita, Kocha Jurgen Klopp na jeshi lake litakuwa na kazi kubwa ya kutetea taji hilo kwa msimu huu.

Mambo yalikuwa moto kabisa kwenye kikosi hicho mwanzoni mwa msimu. Desemba 19, 2020 chama hilo la Anfield lilichapa Crystal Palace, mabao 7-0 uwanjani Selhurst Park na kujikita kileleni kwa tofauti ya pointi nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.

Lakini, miezi miwili baadaye - kila kitu kimebadilika na wachambuzi wa mambo ya soka pamoja na mashabiki wa mchezo huo, wanaitambua Liverpool kama mabingwa watetezi wa ovyo zaidi kwenye Ligi Kuu England baada ya kuchapwa 2-0 na Everton kwenye kipute cha Merseyside derby, uwanjani Anfield wikiendi iliyopita.

Je, ni kweli Liverpool ni mabingwa watetezi wa ovyo zaidi kwenye Ligi Kuu England?

Majibu si kweli. Liverpool si mabingwa watetezi wa ovyo zaidi kwenye Ligi Kuu England.

Hata hawapo kwenye nafasi ya pili ya mabingwa watetezi wa ovyo kwenye historia ya Ligi Kuu England, namba hizo zina wenyewe.

Leicester City ya msimu wa 2016-17 ilikuwa bingwa mtetezi wa ovyo zaidi kwenye Ligi Kuu England kutokana na rekodi zao za uwanjani. Leicester City kwa msimu huo, ikiwa bingwa mtetezi kwenye ligi, kwenye mechi 25 za mwanzo katika ligi, ilishinda tano tu na kuchapwa 14.

Hali ilikuwa mbaya na mwisho wa msimu walimaliza nafasi ya 12.

Chelsea ya msimu wa 2015-16 kikosi chao kilikuwa na namba za ovyo kabisa ndani ya uwanja na huo ndio msimu uliomshuhudia Jose Mourinho akifutwa kazi kwenye kikosi hicho cha Stamford Bridge kwa mara ya pili.

Chelsea ilikuwa bingwa mtetezi wa Ligi Kuu England wa ovyo namba mbili baada ya Leicester City.

Msimu huo, The Blues ilishinda mechi saba tu kati ya 25 za mwanzo, ikipoteza mara tisa na ilimaliza nafasi ya 10 kwenye ligi ilipofika mwisho.

Liverpool hii ya msimu huu 2020-21 inashika namba tatu kwa kuwa mabingwa watetezi wa ovyo zaidi kwenye Ligi Kuu England, ikiwa imeshinda mechi 11 na kuchapwa saba katika mechi 25 ilizocheza hadi sasa.

Hata hivyo, licha ya kwamba si mabingwa watetezi, lakini bado kuna wasiwasi mkubwa wa kiwango cha Liverpool.

Kwa mfano, kikosi hicho cha Liverpool kiwango chake ni cha ovyo kuliko ile Manchester United iliyokuwa inatetea ubingwa wao wa ligi msimu wa 2013-14 chini ya Kocha David Moyes.

Moyes, maarufu ‘Chosen One’ alikabidhiwa Man United kutoka kwa Sir Alex Ferguson baada ya kustaafu, hata hivyo, alifutwa kazi katika msimu wake huo huo wa kwanza Old Trafford.

Hata hivyo, Man United ilikuwa imeshinda mechi 12 kati ya 25 za mwanzo, moja zaidi ya Liverpool kwa msimu huu.

Kwa Liverpool na mwendo wao wa msimu huu kuna visingizio vingi, wamekuwa wakisumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara ya wachezaji wao muhimu.

Kocha Jurgen Klopp amewapoteza mabeki wake mahiri kabisa Virgil van Dijk na Joe Gomez mwanzoni wa msimu, kabla ya beki mwingine Joel Matip kuumia pia, huku wale waliokuwa wakitumika kuziba mapengo ya mabeki hao, viungo Jordan Henderson na Fabinho nao kuumia.

Miamba hiyo ya Anfield imeshuhudia pia wachezaji wake muhimu kikosi cha kwanza, Diogo Jota, Naby Keita na James Milner wakiumia, huku Klopp akitumia pacha 18 tofauti za mabeki wa kati kutokana na janga hilo la majeruhi katika kikosi chake.