Mpo? Mbappe, Haaland kushushwa huko Barcelona

BARCELONA, HISPANIA

MGOMBEA urais wa klabu ya Barcelona, Toni Freixa ameahidi kwamba atafungua pochi kufanya usajili wa mastaa kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kama atachaguliwa, huku Erling Haaland na Kylian Mbappe wakiwa kwenye mipango yake.

Mashabiki wa Barcelona watapiga kura Machi 7 kuamua nani awe rais wao mpya wa kuwaongoza kati ya Freixa, Joan Laporta na Victor Font. Na Freixa anajaribu kuwavutia wapigakura kwa kusisitiza kwamba atatoa mkwanja wa Pauni 216 milioni kufanya usajili ili kuboresha kikosi chao.

Akizungumza na radio RAC-1, Freixa alisema: “Tutakuwa na kikosi cha kiushindani zaidi kwa msimu wa 2021-22. Hatuwezi kuwataja wachezaji hadi hapo tutakapowasajili.”

Lakini, alipoulizwa kuhusu washambuliaji wawili bora kabisa duniani kwa sasa, alisema: “Inawezakana kuwaleta Haaland na Mbappe.”

Mbappe aliifanya vibaya Barcelona kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati alipofunga hat-trick uwanjani Nou Camp. Haaland, naye kwa upande wake amekuwa moto kwelikweli huko Borussia Dortmund ambapo amefunga mabao 27 katika mechi 25 alizocheza msimu huu.

Real Madrid inawataka wachezaji wote hao wawili - hiyo ina maana kwamba miamba hiyo vita yao ya El Clasico itahamia kwenye kunasa saini za washambuliaji hao.

Liverpool nao wamekuwa wakihusishwa na Mbappe, wakati Haaland ametajwa kuwa kwenye rada za Chelsea na miamba miwili ya Manchester - Manchester United na Manchester City.

Sambamba na mpango huo wa kunasa washambuliaji hao matata, Freixa amepanga pia kusajili mabeki wawili watue kwenye kikosi. David Alaba na Eric Garcia, ambao wote watakuwa wachezaji huru mwishoni mwa msimu huu, wanatajwa kwamba watakuwa kwenye mpango huo, licha ya Alaba kutaka alipwe mshahara wa Pauni 400,000 kwa wiki.

Mastaa hao wapya wanne wakitua kwenye kikosi, hiyo ina maana, Barcelona itakuwa balaa kwa msimu ujao.