Carragher: Slot akikwama hapa hana kazi tena
Muktasari:
- Mabingwa hao wamepata anguko kubwa la kiwango msimu huu na hawajashinda mchezo wowote katika mechi tano za mwisho, hali inayoonyesha wapo kwenye kipindi kibaya zaidi.
LIVERPOOL,ENGLAND: JAMIE Carragher anatabiri Liverpool itamfuta kazi Arne Slot endapo atashindwa kuipeleka klabu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mabingwa hao wamepata anguko kubwa la kiwango msimu huu na hawajashinda mchezo wowote katika mechi tano za mwisho, hali inayoonyesha wapo kwenye kipindi kibaya zaidi.
Kwa sasa, Liverpool imeshuka hadi chini ya wapinzani wao Manchester United na Chelsea kwenye msimamo wa ligi na iko hatarini kukosa nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Iwapo Liverpool itashindwa kufuzu kwenye mashindano hayo makubwa barani Ulaya, Carragher anaamini Slot ataondolewa kazini huko Anfield.
Akizungumza kwenye kipindi cha Monday Night Football cha Sky Sports, Carragher amesema: “Ukianza kuona kile ambacho Manchester United wamefanya katika wiki chache zilizopita, ukianza kuwaona Chelsea na ukitazama ni nafasi gani Liverpool inaweza kumaliza nje ya maeneo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, hapo ndipo unaanza kuwa na hofu.
“Hapo ndipo mjadala kuhusu kazi ya kocha unabadilika kabisa. Hilo ni jambo tofauti kabisa. “Kama tunazungumzia kutoshinda ligi au kutokuwa kwenye mbio za ubingwa, hilo ni jukumu la pamoja na Liverpool hawashindi ligi kila msimu. Lakini kukosa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuwa mabingwa, kutumia Pauni 450 milioni kwenye usajili na kuwa na bili ya mishahara ya juu zaidi, nadhani hapo kuna maswali mazito sana. Kama hawatafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushinda ligi msimu uliopita na kutumia pesa nyingi kiasi hicho, sioni kama ana hoja yoyote ya kujitetea.”
Kumekuwa na tetesi kwamba kufukuzwa kwa Slot kunakaribia, huku Liverpool ikitajwa kuwa tayari kumteua gwiji wa klabu hiyo Steven Gerrard kama kocha wa muda kuchukua nafasi yake. Hata hivyo, Slot haonekani kuwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wake wa ajira yake anaamini atapewa muda wa kurekebisha hali.