Carragher ataja mziki wake Ligi Kuu England
Muktasari:
- Beki huyo wa zamani wa Liverpool, ambaye pia ni mchambuzi wa soka kwenye televisheni ya Sky Sports alitangaza kikosi hicho wakati wa mechi ya ligi, Fulham ilipoichapa Nottingham Forest 1-0 usiku wa Jumatatu iliyopita.
LONDON, ENGLAND: JAMIE Carragher hakuwa na namna zaidi ya kuwaomba radhi mashabiki wa Chelsea kutokana na kile alichokifanya cha kutangaza kikosi chake bora cha msimu kwenye Ligi Kuu England hadi sasa.
Beki huyo wa zamani wa Liverpool, ambaye pia ni mchambuzi wa soka kwenye televisheni ya Sky Sports alitangaza kikosi hicho wakati wa mechi ya ligi, Fulham ilipoichapa Nottingham Forest 1-0 usiku wa Jumatatu iliyopita.
Carragher wakati anataja kikosi chake aliwafikiria wachezaji 11 ambao yeye anaamini wamekuwa na viwango bora kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Golini, Carragher aliamua kumchagua kipa wa Sunderland, Robin Roefs.
Kwenye safu ya ulinzi, Carragher amewapanga wakali wawili wa Crystal Palace, Daniel Munoz na Marc Guehi ambapo watachezaa sambamba na wakali wengine wawili wa Arsenal, Gabriel Magalhaes na Riccardo Calafiori katika ukuta wake wa mabeki wanne. Mchezaji wa tatu wa Arsenal, yupo kwenye safu ya kiungo, ambaye ni Declan Rice.
Kwenye eneo hilo la kati ya uwanja, Rice atacheza sambamba na kiungo wa Sunderland, Granit Xhaka na nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes.
Katika eneo la ushambuliaji, gwiji huyo wa Ligi Kuu England amempanga straika wa Manchester City, Erling Haaland katikati, huku mawinga wake, upande mmoja atakuwa staa wa Bournemouth, Antoine Semenyo na ule mwingine atakuwa mkali wa Aston Villa, Morgan Rogers.
Mchezaji mmoja ambaye amekosekana kwenye kikosi hicho cha Carragher, ambaye wengi wangependa kuona anamtaja kutokana na kiwango chake cha msimu huu ni kiungo wa Chelsea, Moises Caicedo, ambaye inaaminika ni Namba 6 bora kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Na hilo ndilo linalomfanya Carragher kuwaomba radhi mashabiki wa Chelsea.
Carragher alisema: “Nadhani Declan Rice amemzidi Caicedo. Pia naona mchango wa Xhaka msimu huu, amekuwa na kitu kwenye timu yake. Ni muhimu huko Sunderland. Nawaomba radhi mashabiki wa Chelsea, hakuna nafasi ya Caicedo.”
Lakini, mashabiki hawakufurahishwa na hilo, ambapo mmoja alisema: “Hiki ni kikosi cha hovyo kabisa.”
Mwingine aliandika: “Yuko wapi Reece James?”
Mwingine aliongeza: “Msichukulie siriazi.”