Carragher afuta kauli yake kwa Casemiro
Muktasari:
- Miaka miwili baada ya ukosoaji wake uliovuma dhidi ya kiungo huyo raia wa Brazil, Carragher amefanya mabadiliko ya msimamo wake kuhusu kauli yake kali.
MANCHESTER, ENGLAND: JAMIE Carragher hatimaye amekiri soka halijamwacha nyota wa Manchester United, Casemiro, kama alivyodai hapo awali.
Miaka miwili baada ya ukosoaji wake uliovuma dhidi ya kiungo huyo raia wa Brazil, Carragher amefanya mabadiliko ya msimamo wake kuhusu kauli yake kali.
Kauli hiyo inakuja baada ya Casemiro, ambaye tayari ametangaza ataondoka Manchester United mwishoni mwa msimu huu, kufunga bao na kuasisti katika ushindi wa kusisimua wa mabao 3-2 dhidi ya Fulham kwenye Uwanja wa Old Trafford, Jumapili.
Mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid alianza kwa kufunga bao la kwanza kwa kichwa, kabla ya kumtengenezea Matheus Cunha bao la pili la Mashetani Wekundu.
Uchezaji wa Casemiro umeisaidia Man United kushinda mechi zote tatu walizocheza chini ya kocha mpya Michael Carrick, huku kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33 akiwa mhimili muhimu wa mafanikio hayo. Hii ni tofauti kubwa na kiwango alichokuwa akionyesha mwishoni mwa msimu wa 2023/24.
Baada ya Man United kufungwa mabao 4-0 na Crystal Palace chini ya kocha Erik ten Hag mnamo Mei 2024, Carragher amesema: “Nadhani Casemiro anapaswa kujua leo usiku anapaswa kubakiwa na mechi tatu pekee za kucheza katika kiwango cha juu. Mechi mbili zijazo za ligi na fainali ya kombe, kisha aanze kufikiria kwenda MLS au Saudi Arabia. Hili lazima likome kwa sababu tunashuhudia mmoja wa wachezaji wakubwa wa kisasa. Kila mara nakumbuka msemo unaosema, ‘acha soka kabla soka halijakuacha’. Soka limemwacha. Katika kiwango hiki cha juu, anapaswa kufikia tamati na kuondoka.”
Miaka miwili baadaye, Casemiro ameendelea kuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Man United, Carragher amekiri alikosea.
Akizungumza na Sky Sports, Carragher amesema: “Sasa ni haki kusema soka halijamwacha. Ukiangalia anachokifanya msimu huu katika Ligi Kuu na siyo tu dhidi ya Fulham nyumbani, bali pia kile alichokifanya wiki iliyopita dhidi ya Arsenal ugenini na Manchester City nyumbani.
"Casemiro ana haki kabisa, kama angependa kunijibu na kusema, ‘acha uchambuzi kabla uchambuzi haujakuacha!’ Angeweza kabisa kunirudishia kauli hiyo. Nampongeza, anaonekana kuwa mchezaji tofauti kabisa. Hata kimwili, anaonekana tofauti. Hata niliposema yale maneno, alikuwa anaonekana kama mchezaji aliyekuwa karibu kumaliza muda wake. Iwe alijiachia kidogo au sasa amekuwa mtaalamu sana kimwili, anaonekana tofauti kabisa.”