Bruno Fernandes adai mkewe anamkosoa sana
Muktasari:
- Nahodha huyo wa Manchester United, Fernandes anatazamwa kama mmoja wa wachezaji bora kabisa waliowahi kutokea kwenye kikosi hicho tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu 2013.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO Bruno Fernandes amefichua mkosoaji wake mkubwa ni mkewe, mrembo Ana Pinho.
Nahodha huyo wa Manchester United, Fernandes anatazamwa kama mmoja wa wachezaji bora kabisa waliowahi kutokea kwenye kikosi hicho tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu 2013.
Fernandes alishinda tuzo ya Sir Matt Busby kwa maana ya mchezaji bora wa mwaka kwenye kikosi cha Man United mara nne na anashika namba 20 kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika kikosi cha Old Trafford.
Fernandes, 31, amekuwa akikosolewa na wachambuzi wa soka kibao kutokana na kulalamika sana kwa waamuzi na yale maigizo yake ya kugalagala kama ameumia sana wakati atakapongushwa uwanjani.
Lakini, Fernandes abainisha mkewe, mrembo Ana Pinho, ndiye mtu anayemkosoa zaidi kuliko wote.
Fernandes amesema: “Nadhani kuwa na mke nyumbani ni kitu kizuri sana kwa sababu ananikosoa sana. Ninaporudi nyumbani na kama umefunga bao au kufanya kitu chochote kile, basi atakukosoa kama alivyokuwa akifanya baba yangu nilipokuwa mdogo.
“Unatoka kwenye mechi, unaweza kuwa ulifunga bao, lakini yeye ukirudi utamsikia, hivi ulipotezaje ule mpira? Wakati mwingine namwambia, hivi hunisifii japo mara moja? Wakati mwingine narudi na tuzo ya mchezaji bora wa mechi, utamsikia akisema ‘ulikuwa mchezaji bora wa mechi?’ Ni kama vile yeye anaona sikucheza vizuri.”
Katika mahojiano yake mwingine aliyofanya hivi karibuni, kiungo Fernandes alibainisha kuumizwa na namna mabosi wa Man United walivyofikiria kumpiga bei kwenda klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi wakati miamba hiyo ya Arabuni ilipopeleka ofa huko Old Trafford kwa ajili ya kunasa saini ya Mreno huyo.