Bro'ake Mainoo aleta uchochezi
Muktasari:
- Staa huyo wa zamani wa Love Island, Jordan Mainoo-Hames alipigwa picha akiwa amevaa fulana nyeusi iliyokuwa na maandishi 'Free Kobbie Mainoo' kifuani yaliyoandikwa kwa rangi nyeupe.
MANCHESTER, ENGLAND: KAKA yake kiungo Kobbie Mainoo amechukua uamuzi wa kuvaa fulana yenye maandishi ya uchochezi wakati wa mechi ya Manchester United iliyomalizika kwa sare ya mabao 4-4 dhidi ya Bournemouth, uwanjani Old Trafford usiku wa Jumatatu.
Staa huyo wa zamani wa Love Island, Jordan Mainoo-Hames alipigwa picha akiwa amevaa fulana nyeusi iliyokuwa na maandishi 'Free Kobbie Mainoo' kifuani yaliyoandikwa kwa rangi nyeupe.
Kundi fulani la mashabiki wa Man United walitumia saa kadhaa kabla ya mechi hiyo kuanza kufanya maandamano kutokana na Mainoo kutopewa muda wa kutosha wa kucheza chini ya Kocha Ruben Amorim.
Mainoo alijikuta benchini katika mechi hiyo na kocha aliendelea kuwapa kipaumbele viungo Bruno Fernandes na Casemiro. Katika mechi dhidi ya Bournemouth, Mainoo aliamsha shangwe ya mashabiki na kumshangilia wakati alipokuwa akiiingia kuchukua nafasi ya Casemiro wakati huo Man United ikiwa nyuma kwa mabao 3-2.
Mainoo amekuwa akihusishwa na mpango wa kuondoka kwa mkopo Man United dirisha la uhamisho wa Januari baada ya kuichezea timu hiyo dakika 302 kwenye Ligi Kuu England, huku akianzishwa mara 19 katika mechi 25 alizocheza msimu wa 2024/25. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20 kipenzi cha mashabiki hajajumuishwa kwenye kikosi cha kwanza katika mechi 16 za ligi msimu huu na jambo hilo linazifanya timu za Napoli na Chelsea kuhitaji huduma yake.
Mainoo anataka kupewa muda wa kucheza, lakini Man United inamtaka abaki kwa sababu Noussair Mazraoui, Bryan Mbeumo na Amad Diallo watapungua kikosini kwa sababu watakwenda kuungana na timu zao za taifa za Afrika kwa ajili ya mashindano ya Afcon 2025 huko Morocco.
Sasa, kaka yake ameamua kulishikia bango suala hilo akimtaka mdogo wake apewe kile anachotaka ili kuondoka kwenye manyanyaso ya kocha Amorim. Mainoo-Hames aliposti picha yake yenye maandishi hayo mbele ya wafuasi wake 681,000 kwenye Instagram. Uamuzi huo wa kaka yake Mainoo haujaleta shida yoyote, kwani kiungo huyo alikuwa na wakati mzuri wakati alipoingia katika mechi hiyo ya sare dhidi ya Bournemouth.
Casemiro hatacheza mechi ijayo ya Man United dhidi ya Aston Villa baada ya kuonyeshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Marcus Tavernier na kusababisha mpigo wa mpira wa adhabu ambao ulimshinda kipa Senne Lammens na kutinga nyavuni. Kutokana na hilo, Mainoo anapewa nafasi kubwa ya kucheza katika mechi hiyo ya Aston Villa, Jumapili ijayo hasa ukizingatia Amad, Mbeumo na Mazraoui watakuwa wamekwenda kwenye majukumu ya Afcon.
KLABU SABA ZINAZOTAJWAKUMSAKA KOBBIE MAINOO
1.Napoli, Italia
2.Chelsea, England
3.Real Madrid, Hispania
4.Bayern Munich, Ujerumani
5.Barcelona, Hispania
6.Newcastle, England
7.West Ham, England