BRAZIL 2014: TUNATISHA: Algeria yaua, Mkenya aibeba Ubelgiji

Beki wa Algeria,Rafik Halliche akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao la pili dhidi ya Korea Kusini.
Muktasari:
- Wanachotakiwa kukifanya Algeria ni kuifunga Urusi inayonolewa na kocha wa zamani wa England, Fabio Capello katika mechi yao ya Alhamisi ili wakate tiketi ya kucheza hatua ya pili baada ya kulala kwa 2-1 mbele ya Ubelgiji katika mechi ya kwanza.
PORT ALEGRE, BRAZIL
WAWAKILISHI wa Afrika, Algeria imefufua matumaini ya kufuzu hatua ya pili ya fainali za Kombe la Dunia baada ya kuichapa Korea Kusini mabao 4-2 katika mechi ya Kundi H iliyochezwa jana Jumapili usiku.
Wanachotakiwa kukifanya Algeria ni kuifunga Urusi inayonolewa na kocha wa zamani wa England, Fabio Capello katika mechi yao ya Alhamisi ili wakate tiketi ya kucheza hatua ya pili baada ya kulala kwa 2-1 mbele ya Ubelgiji katika mechi ya kwanza.
Algeria inayoshika nafasi ya pili katika kundi lake, ina kumbukumbu za kumbania Capello katika fainali za Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini wakati huo Capello akiinoa England na kutoka nayo sare ya 0-0 na bila shaka itaingia uwanjani ikiwa na matumaini ya kumfanyia Capello kile ilichomfanyia 2010 ingawa safari hii kocha huyo atakuwa na timu ya Urusi.
Algeria jana iliandika bao lake la kwanza dakika ya 25 lililofungwa na Islam Slimani kwa shuti la mguu wa kushoto kabla ya kuandika la pili dakika mbili baadaye lililofungwa kwa kichwa na Rafik Halliche.
Bao la tatu la Algeria lilifungwa na Abdelmoumene Djabou dakika ya 37 lakini dakika tano baada ya kipindi cha pili, Korea Kusini walipata bao la kwanza lililofungwa na Son Heung-Min.
Algeria nao walizinduka na kuandika bao la nne dakika ya 62 mfungaji akiwa ni Yacine Brahimi wakati bao la pili la Korea lilifungwa na Koo Ja-Cheol kwa shuti la mguu wa kushoto dakika ya 72.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo, bao la Divock Okoth Origi alilofunga dakika mbili kabla ya mpira kumalizika liliisaidia Ubelgiji kuilaza Urusi na kufuzu hatua ya pili ya fainali za Kombe la Dunia.
Origi anayeichezea Lille ya Ufaransa na ambaye ndio kwanza ana miaka 19 jana aliingia dakika ya 57 badala ya Romelu Lukaku, alifunga bao hilo akiitumia vyema krosi ya Eden Hazard na kuujaza mpira kimiani kwa shuti la mguu wa kulia.
Mchezaji huyo ambaye asili yake ni Kenya ingawa alizaliwa Ubelgiji, baba yake, Michael Okoth ‘Mike’ Origi alikuwa mwanasoka na aliwahi kuichezea Shabana na timu kadhaa za Kenya kabla ya kutimkia Ubelgiji alikotamba na Racing Genk.
Kwa ushindi huo, Ubelgiji ambayo katika dakika ya 31 ilimpoteza beki wake ambaye pia anaichezea Arsenal, Thomas Vermaelen aliyeumia, imefikisha pointi sita katika mechi mbili.
Kwa bao hilo ni wazi kwamba Origi atakuwa ameishawishi zaidi Tottenham ambayo inadaiwa kuwa katika mpango wa kumsajili.
Hata hivyo ili iweze kufika mbali zaidi, Ubelgiji, yenye wakali wengine kama Marouane Fellaini, Vincent Kompany, Daniel Van Buyten na kipa wa Chelsea anayeichezea Atletico Madrid kwa mkopo, Marc Courtois ina kazi ya kufanya kwa kuwa soka lake bado halijavutia wengi.