BRAZIL 2014: Kwanini Brazil ilifungwa mabao saba?

Muktasari:
Hakukuwa na maajabu yoyote zaidi ya mbinu mbovu za Kocha, Luis Fillipe Scolari. Katika soka la kisasa unaweza kufungwa mabao mengi ndani ya dakika chache tu kama kocha anatumia mbinu mbovu dhidi ya timu makini kama Ujerumani.
HAKUNA uchawi katika soka la kisasa. Uwe ulilitazama pambano la Brazil na Ujerumani ukiwa Tanzania au hapa Brazil, ilikuwa rahisi kugundua kwa nini Brazil imefungwa mabao 7-1 na Ujerumani.
Hakukuwa na maajabu yoyote zaidi ya mbinu mbovu za Kocha, Luis Fillipe Scolari. Katika soka la kisasa unaweza kufungwa mabao mengi ndani ya dakika chache tu kama kocha anatumia mbinu mbovu dhidi ya timu makini kama Ujerumani.
Wakati pambano linaanza, Scolari alikuwa ana wachezaji wawili tu eneo la kiungo ambao ndio aliwaamini kuleta uwiano katika ulinzi na mashambulizi.
Alikuwa na Luiz Gustavo na Fernandinho.
Wengine pale mbele walikuwepo Oscar, Bernard, Hulk na Fred. Lilikuwa jambo la hatari sana kwa sababu wote hawa wana mawazo ya kushambulia zaidi kuliko kujihami.
Mbaya zaidi kwa Scolari, alikuwa anacheza na timu yenye viungo maridadi ambao klabu zao mbili; Bayern Munich na Borussia Dortmund, zimetesa mno barani Ulaya katika miaka ya karibuni.
Unacheza dhidi ya Ujerumani iliyojaza viungo wengi katikati akina Thomas Muller, Bastian Shweinsteiger na Toni Kroos. Hapo hapo kuna Mesut Ozil wa Arsenal na Sami Khedira wa Real Madrid. Unategemea nini zaidi?
Scolari alipaswa kucheza kama kibonde katika mechi hii. Alipaswa kwanza kuichunga Ujerumani na si kuanza kuwashambulia kwa kasi kama alivyofanya ndani ya dakika tano za mwanzo. Lilikuwa kosa kubwa.
Kinachozungumzwa ni kwamba Scolari alikuwa anatafuta bao la mapema na kisha timu yake irudi nyuma kwa ajili ya kujihami na kucheza kwa umakini.
Bahati mbaya bao lenyewe la kwanza halikuangukia katika nyavu za Ujerumani, liliangukia katika nyavu zao.
Bao lenyewe halikuingia kwa staili ya kuonewa. Ulikuwa mpira wa kona. Lakini baada ya hapo kikosi chake kikazidi kufunguka kwa tamaa ya kusaka mabao ya kusawazisha.
Ni hapo ndipo kulionekana daraja kubwa eneo la katikati la Brazil. Fernandinho na Gustavo wasingeweza kuifanya kazi hii peke yao. Kulihitaji viungo wa kulibana eneo la katikati kwa ajili ya kuwabana Wajerumani.
Matokeo yake, unaweza kuwalaumu mabeki wa Brazil, lakini tangu lini kazi ya ulinzi katika soka la kisasa ikafanywa na mabeki peke yao? Matokeo yake ndio yale tuliyoyaona. Wachezaji wa Ujerumani walijikuta wanakabiliana na Dante na David Luiz kwa idadi sawa pindi akina Kroos walipokuwa wakiwavuka akina Bernard na kisha Gustavo.
Mpaka mapumziko kulikuwa na mabao matano. Lakini baada ya hapo nilijua kungekuwa na mabao zaidi kwa sababu Scolari na wachezaji wake walikuwa wameenda vyumba vya kubadilishia nguo wakijidanganya kuwa walipaswa kufunga walau mabao mawili matatu kupunguza aibu.
Lakini kumbe katika soka la kisasa, adui anafurahi zaidi kushambuliwa kwa sababu anapata nafasi ya kufanya mashambulizi ya kushitukiza. Ndicho kilichotokea kwa bao la sita na la saba.
Hili lilikuwa kosa la kwanza la Scolari. Mbinu za uwanjani. Lakini kosa la pili la Scolari na la Wabrazili wote lilikuwa ni kuathirika kisaikolojia kwa kuwakosa Thiago Silva na Neymar.
Baada ya miaka mingi ya kuwepo kwa vizazi vya wachezaji wengi mahiri kiasi kwamba hata ungemchukua muuza nyanya basi angeweza kuichezea timu ya taifa ya Brazil, kwa sasa inaonekana zama hizo zimepita na vipaji vinakauka Brazil.
Ilionekana wazi kwamba wachezaji wawili ambao wangechukua nafasi za
Thiago na Neymar walikuwa hawafikii walau robo ya wenzao. Nchi nzima ikaathirika kisaikolojia huku vyombo vyao vya habari vikilialia tu.
Zamani maisha hayakuwa hivi Brazil. Ni kama ambavyo miaka miwili iliyopita maisha hayakuwa hivi Hispania. Yeyote angeweza kucheza na angeweza kuibeba nchi. Ni kama ilivyo Ujerumani kwa sasa.
Lakini utegemezi kwa Neymar na Thiago ulionekana kupitiliza kiasi kwamba vyombo vya habari vya hapa vilionyesha kuwa Brazil haiwezi kwenda bila ya wao. Lilikuwa kosa kubwa la kiakili na liliwapa nguvu kubwa ya kisaikolojia Wajerumani.
Siamini kama Wajerumani wa sasa wanaweza kulialia kama Muller na Kroos wakikosekana uwanjani. Wengine watacheza na wataonyesha uwezo wao.
Scolari alishindwa kuitengeneza Brazil inayotegemea kucheza kitimu na badala yake ameijenga Brazil inayotegemea majina ya watu.
Hakuna kitu cha kushangaa sana kutokana na kichapo hiki. Ungetazama mechi za Brazil dhidi ya Croatia, Cameroon, Mexico, Chile na Colombia, ilikuwa wazi kwamba kipigo hiki kilikuwa kinawanyemelea. Hata wangecheza na Uholanzi, bado kingewakumba hata kama idadi ya mabao isingekuwa hii.