Branthwaite aziingiza vitani Liverpool, Man U
Muktasari:
- Jarrad mwenye umri wa miaka 22, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Licha ya utayari wa Liverpool, uwezekano wa kuipata saini yake unaonekana kuwa mdogo kutokana na upinzani uliopo baina yao na Everton.
LIVERPOOL ipo tayari kupambana jino kwa jino na Manchester United katika harakati za kuwania saini ya beki wa kati wa Everton, Jarrad Branthwaite katika dirisha lijalo la majira ya baridi.
Jarrad mwenye umri wa miaka 22, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Licha ya utayari wa Liverpool, uwezekano wa kuipata saini yake unaonekana kuwa mdogo kutokana na upinzani uliopo baina yao na Everton.
Mabosi wa Liverpool wanataka kumsajili staa huyo kama sehemu ya kujiandaa na maisha bila ya Virgil van Dijk ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Man United ilishindwa kukamilisha mchakato wa kumsajili Branthwaite katika dirisha lililopita kutokana na kiasi kikubwa cha pesa kilichohitajiwa na mabosi wa Everton.
Mkataba wa sasa wa beki huyu unatarajiwa kumalizika ifikapo 2027 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi mbili za michuano yote.
MKATABA mpya wa Newcastle United wanaotaka kumsainisha winga raia wa England, Anthony Gordon, 23, utakuwa wa miaka sita na utamalizika 2030.
Awali, Gordon ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika ifikapo 2026, tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi nane za michuano yote.
KIUNGO wa Crystal Palace na England, Adam Wharton, 20, na kiungo raia wa Brazil anayeichezea Atalanta, Ederson ni miongoni mwa wachezaji wengine ambao Manchester City inataka kuwasajili katika dirisha la majira ya baridi mwakani ili kuziba pengo la kiungo raia wa Hispania, Rodri, 28, ambaye amepata majeraha yatakayomweka nje kwa msimu mzima.
MANCHESTER United imefikia patamu katika mazungumzo na winga raia wa Ivory Coast, Amad Diallo, 22, juu ya kumuongezea mkataba mpya wakati ule wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.Kocha wa Man United, Erik Ten Hag anaamini Diallo ni mmoja wa wachezaji vijana watakaoisaidia timu hiyo siku za usoni kutokana na maendeleo yake.
KOCHA wa Everton, Sean Dyche anadaiwa kuwahimiza mabosi wa timu hiyo kuhakikisha wanamsajili kipa wa Newcastle United, Nick Pope, 32, katika dirisha lijalo la majira ya baridi kwa ajili ya kumpa changamoto Jordan Pickford, 30, ambaye amekuwa katika kiwango kibovu tangu kuanza kwa msimu huu. Dyche amechukizwa na Pickford kuruhusu mabao kirahisi.
STRAIKA wa Eintracht Frankfurt na Misri, Omar Marmoush, 25, yupo kwenye rada za timu kibao England zinazomtaka katika dirisha lijalo la majira ya baridi baada ya kuvutiwa na kiwango alichoonyesha kuanzia msimu uliopita na huu ulioanza. Miongoni mwa timu zilizoonyesha uhitaji na huduma yake ni Liverpool, Arsenal, Crystal Palace na West Ham United.
REAL Madrid imetuma maskauti wake kwenda Ujerumani kwa ajili ya kumtazama beki wa RB Leipzig na Ufaransa, Castello Lukeba, 21, katika dirisha la majira ya baridi au kiangazi mwaka huu kwa ajili ya kuboresha eneo la ushambuliaji. Kocha wa Madrid, Carlo Ancelotti moja kati ya maeneo ambayo alitaka kuboreshwa msimu huu ilikuwa ni uzuiaji ambapo ilikuwa asajiliwe Leny Yoro kabla ya Manchester United kumbeba.
BEKI wa zamani wa Real Madrid, Sergio Ramos, 38, anadaiwa kuwa katika mpango wa kutua Saudi Arabia baada ya kukataa dili la kwenda Marekani na Brazil.Wawakilishi wa Ramos walikuwa Brazil kwa wiki kadhaa wakijaribu kufanya mazungumzo na timu mbalimbali, lakini ilishindikana kufikia mwafaka kwa sababu ya mshahara mkubwa anaohitaji beki huyo ambaye amefunga mabao zaidi ya 100.