Bosi Spurs aibukia kesi ya Man city
Muktasari:
- Februari 2023, Ligi Kuu England ilifungua mashtaka dhidi ya Man City kuhusu kufanya makosa 115 ya ukiukwaji wa kanuni ya mapato na matumizi katika kipindi cha miaka tisa kati ya 2009 na 2017.
LONDON, ENGLAND: MWENYEKITI wa klabu ya Tottenham Hotspur, Daniel Levy amesema uchunguzi wa madai ya Manchester City kufanya udanganyifu kwenye matumizi ya pesa kwenye usajili unachukua muda mrefu sana.
Februari 2023, Ligi Kuu England ilifungua mashtaka dhidi ya Man City kuhusu kufanya makosa 115 ya ukiukwaji wa kanuni ya mapato na matumizi katika kipindi cha miaka tisa kati ya 2009 na 2017.
Zaidi ya miaka miwili baadaye, hukumu ya sakata hilo bado haijafahamika. Hivi karibuni ilielezwa pengine Oktoba mwaka huu mambo yatafahamika, ni upande gani ulioibuka na ushindi kati ya Ligi Kuu England au Man City. Klabu wapinzani wa Man City Ligi Kuu England zimekuwa kimya tangu mchakato wa kesi hiyo uliposogezwa mbele, lakini bosi wa Spurs, Levy amekuwa miongoni mwa maofisa wakuu wachache waliozungumzia hilo hadharani. Tangu ilipotiwa hatiani, Man City chini ya kocha Pep Guardiola imekana kutenda makosa na ina ushahidi wa kutosha wa kuwatoa salama kwenye sakata hilo.
Katika mahojiano katika kipindi cha Gary Neville cha Overlap, bosi huyo wa Spurs alisema: “Nadhani itakuwa si sawa kwangu mimi kuzungumzia ishu ya klabu nyingine kwenye Ligi Kuu England, lakini ninachoweza kusema ni mchakato huu umechukua muda mrefu sana.
“Ulipaswa kumalizwa, kwa ajili ya usalama wa mchezo. Kwa bahati mbaya, tumeshindwa kumaliza haraka na kuchukua wanasheria wa nje na watachukua tu pesa nyingi kwenye suala hili.”
Man City imekuwa ikipambana na Ligi Kuu England juu ya mashtaka hayo kwa zaidi ya miezi 30. Februari mwaka huu, Guardiola alisema anatarajia hukumu ingetangazwa wiki chache mbele, lakini tangu wakati huo hakuna tangazo.
Alipozungumza Septemba mwaka jana, kocha Guardiola alisema: “Mnisamehe kwa kusema siku zote nimekuwa nikiitetea timu yangu. Ni kama vile kila mtu haoni kama tunaweza kushushwa daraja, wanataka tutoweke kwenye hii dunia.” Guardiola aliongeza: “Ninachoweza kusema tumekuwa na siku nyingi nzuri kuliko wapinzani wetu na timu maana tunashinda mechi hiyo, hilo halina utata.”
Straika wa Man City, Erling Haaland naye anaamini Man City haina kosa lolote kwenye sakata hilo na ndiyo maana alishawishika kusaini mkataba wa miaka tisa na nusu kuendelea kukipiga kwenye kikosi hicho.