Bosi kubwa Dortmund afunga mjadala wa Haaland, Sancho

Muktasari:

  • IMEISHA hiyo. Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Borussia Dortmund, Hans-Joachim Watzke amesema kwa kusisitiza msimu ujao wa 2021-22 wataendelea na Erling Haaland kwenye kikosi chao.

LONDON, ENGLAND. IMEISHA hiyo. Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Borussia Dortmund, Hans-Joachim Watzke amesema kwa kusisitiza msimu ujao wa 2021-22 wataendelea na Erling Haaland kwenye kikosi chao.

Lakini, amesema kama kutakuwa na ofa ya maana kuhusu winga wa England, Jadon Sancho basi watakubali kukaa mezani dirisha lijalo la kiangazi kufanya biashara.

Hatima ya maisha ya baadaye ya Haaland huko Westfalenstadion imekuwa kwenye shaka kubwa baada ya wakala wake, Mino Raiola, kwa sasa anahangaika kumtafutia timu kwenda kujiunga nayo.

Raiola anaamini Haaland, 20, ameshaonyesha kiwango bora Bundesliga na baada ya miezi 16 kwenye klabu ya BVB anahitaji kupiga hatua nyingine ya juu kisoka.

Na ndio maana wakala huyo na baba wa mchezaji, ambaye ni kiungo wa zamani wa Manchester City, Alf-Inge Haaland, wamekuwa wakikutana na mabosi wa klabu kubwa za Ulaya hususan Barcelona na Real Madrid kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Norway akakipige.

Hata hivyo, Dortmund wameweka wazi na kumwambia Raiola na baba yake Haaland kwamba hawana mpango wa kumuuza mshambuliaji huyo dirisha lijalo la uhamisho wa kiangazi.

Hilo halijalishi kwamba kama wakimuuza mwaka huu watapata mara mbili ya Euro 75 milioni, kiwango kilichowekwa kwenye mkataba wake kama atauzwa mwakani 2022.

Lakini, Watzke haamini kama kuna klabu Ulaya kwa sasa itakuwa tayari kulipa pesa nyingi kiasi hicho kwenye dirisha lijalo la uhamisho kutokana na timu nyingi kutikiswa kiuchumi na janga la virusi vya corona. Na kutokana na hilo, Dortmund haifikirii kumuuza Namba 9 wao huyo mwaka huu.

“Hatuwezi kuwa na mpango unaofanana. Tunajadili hili na Erling, baba yake na wakala wake Mino Raiola,” alisema Watzke alipozungumza na DAZN . “Tunahitaji pia kumwona akiwa mwenye furaha wakati anabaki kwetu, kuendelea kuifungia mabao BVB mwakani. Hakuna mpango mbadala.”

Sancho, ambaye angeweza kunaswa na Manchester United kama Dortmund ingepunguza bei ya Pauni 108 milioni Agosti mwaka jana, habari yake ni tofauti.

Alizungumzia kama Haaland na Sancho wote wataendelea kubaki Dortmund msimu wa 2021-22, Watzke alisema: “Sitaki kuingia kwenye mambo ya nadhania, si kitu kizuri. Jadon Sancho amekuwa na sisi kwa muda mrefu kuliko Erling Haaland. Tutazungumza na Jadon pia. Kama kutakuwa na ofa ya maana mezani, tutajadili hiyo na mchezaji na wakala wake, ipo wazi.

“Hata hivyo, nina hakika dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi halitakuwa na mambo mengi. Hasa kwa hizi klabu kubwa, zimeathiriwa sana na janga la corona na kutikiswa kiuchumi si suala la kumalizwa ndani ya wiki mbili.” Kwa maelezo hayo ya bosi wa Dortmund ni kwamba wataweka ngumu kwenye mauzo ya Haaland mwishoni mwa msimu huu, huku wakifungua milango kwa timu itakayohitaji saini ya Sancho. Barcelona wanahitaji saini ya Haaland, lakini shida iliyopo ni kwamba watalazimika kulipa cha juu Euro 40 milioni, kuwalipa wakala Raiola na baba yake mchezaji huyo, Euro 20 milioni kila mmoja, huku mchezaji mwenyewe akihitaji mkataba wenye thamani ya Euro 30 milioni kwa mwaka. Kwa uchumi huu wa sasa kuna timu yenye uwezo wa kulipa mkwanja huo.

Sancho kwa muda mrefu amekuwa akisakwa na Manchester United, akidaiw akuwa kipenzi kikubwa cha kocha Ole Gunnar Solskjaer, lakini mahasimu wao Manchester City nao wanaweza kuingia kwenye mchakamchaka wa kunasa huduma ya winga huyo wa kimataifa wa England. Kama Sancho atanaswa na timu nyingine, basi Man City itapata asilimia 15 ya pesa atakayokuwa ameuzwa staa huyo, huku Paris Saint-Germain wakipiga hesabu za kwenda kumnasa kama Kylian Mbappe ataamua kuachana na miamba hiyo kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.