Bosi Bayern ampiga kijembe Wirtz
Muktasari:
- Hata hivyo, hilo halikumfanya ajiepushe na vijembe kutoka kwa timu iliyowahi kumfukuzia kutaka saini yake, Bayern Munich.
LIVERPOOL, ENGLAND: KIUNGO, Florian Wirtz amecheza kwa kiwango bora sana aliporejea uwanjani kuitumikia Liverpool kwenye ushindi dhidi ya West Ham United, Jumapili iliyopita akitokea kwenye majeraha yaliyomweka nje kwa siku kadhaa.
Hata hivyo, hilo halikumfanya ajiepushe na vijembe kutoka kwa timu iliyowahi kumfukuzia kutaka saini yake, Bayern Munich.
Kiungo huyo mwenye kipaji cha hali ya juu alizikataa klabu za Bayern Munich na Manchester City kukubali uhamisho wa Pauni 116 milioni kutoka Bayer Leverkusen kwenda kujiunga na Liverpool kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Lakini, Wirtz, 22 alianza kwa kasi hafifu huko Anfield na bado anajitafuta akicheza mechi 17 kwenye kikosi cha Liverpool hadi sasa, hajafunga wala kuasisti kwenye Ligi Kuu England.
Kiwango chake kimekuwa cha kupanda na kushuka na ndiyo maana kocha Arne Slot amekuwa akimwingiza na kumtoa kwenye kikosi chake, huku akitumika kwenye nafasi tofauti uwanjani.
Rais wa heshima wa Bayern Munich, Uli Hoeness amempiga kijembe Wirtz kwa uamuzi wake wa kuichagua Liverpool na kuikacha miamba hiyo ya soka ya Ujerumani. Bayern ilivamia Liverpool dirisha lililopita na kumnasa Luis Diaz, ambaye amekuwa na kiwango bora tangu alipotua Allianz Arena, akiibuka na ushindi kwenye mechi 18 kati ya 20 za michuano yote msimu huu, huku kipigo pekee ni kile cha Arsenal kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki iliyopita.
Hoeness alisema: “Tumethibitisha msimu huu kwamba tunaweza kushindana kwenye ubora wote. Tumewafunga Chelsea, moja ya timu bora duniani. Tuliwafunga PSG na tulishahili kupoteza dhidi ya Arsenal, timu nzuri. Lakini, kama nilivyoeleza Bayern ni moja ya klabu tatu hadi tano bora duniani. Liverpool wao wametumia Euro 500 milioni na imekuwa na msimu wa hovyo. Kwa maoni yangu, hiyo ni kwa sababu imesajili masupastaa tu. Kama nilivyosema, Liverpool sasa itahitaji kucheza na mipira mitano kwa sababu mastaa wao watashindwa kuiachia.
“Maskini Florian Wirtz, hapati mpira kwa sababu Salah na Szoboszlai na wengineo kila mmoja anataka kucheza mpira wake.”
Bayern Munich ilikuwa na nafasi kubwa ya kumsajili Wirtz kabla ya Liverpool kuibuka kumnasa.