Bingwa Saudia kupatikana leo, ni Ronaldo vs Benzema
Muktasari:
- Mashabiki wa soka wanaelekeza macho yao nchini humo kushuhudia dakika 90 zitakazoamua nani atatawazwa kuwa mfalme mpya wa soka la Saudia msimu huu, katika usiku unaotajwa kuwa wa presha kubwa zaidi kwa pande zote mbili.
MCHUANO mkali wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia unafikia tamati leo usiku, huku timu mbili vigogo za Al Nassr anayoitumikia Cristiano Ronaldo na Al Hilal anayocheza Karim Benzema zikiwa kwenye vita kubwa ya kushindania taji hilo.
Mashabiki wa soka wanaelekeza macho yao nchini humo kushuhudia dakika 90 zitakazoamua nani atatawazwa kuwa mfalme mpya wa soka la Saudia msimu huu, katika usiku unaotajwa kuwa wa presha kubwa zaidi kwa pande zote mbili.
Hesabu za ubingwa kwa upande wa Al Nassr ziko wazi kwani ushindi wa aina yoyote kwenye mchezo wa leo dhidi ya Damac utaipa taji hilo moja kwa moja bila kutegemea matokeo ya wapinzani wao.
Hata hivyo, Al Nassr inaweza pia kutangazwa bingwa hata kama itapoteza au kutoka sare, endapo Al Hilal itapoteza au kuambulia sare dhidi ya Al Fayha. Kwa upande mwingine, Al Hilal bado ina nafasi ya kupindua meza dakika ya mwisho na kutwaa ubingwa huo kupitia mazingira mawili.
Kwanza, Al Hilal itakuwa bingwa kama itashinda, huku Al Nassr ikipoteza dhidi ya Damac.
Pili, Al Hilal inaweza kubeba ndoo hata kama Al Nassr itapata sare, endapo yenyewe itashinda kwani itanufaika na sheria ya matokeo ya mechi walizokutana wenyewe kwa wenyewe msimu huu.
Msimamo wa ligi hiyo unaonesha Al Nassr inaongoza ikiwa na pointi 83, ikifuatiwa na Al Hilal yenye 81 sawa na Al Ahli ambayo yenyewe ishamaliza kucheza mechi 34, huku timu hizo mbili zikiwa na mechi 33.