Bilionea aweka mezani Pauni 2 bilioni kuinunua Arsenal

LONDON, ENGLAND. NDO hivyo. Bilionea wa Spotify, Daniel Ek ameibuka kivingine kwenye mpango wake wa kuinunua Arsenal, akiongeza dau na kufikia Pauni 2 bilioni, huku baadhi wa mashabiki wa timu hiyo ya Emirates, akisema “apewe tu.”

Bilionea Ek, ambaye ni shabiki wa Arsenal – ofa yake ya mwanzo ya kununua timu hiyo ilikwama na sasa tajiri huyo raia wa Sweden, amekuja na ofa ya pili na anaamini inaweza kumshawishi mmiliki wa klabu hiyo ya Emirates, Stan Kroenke na kufanya biashara.

Ofa yake ya kwanza ya Pauni 1.8 bilioni ilikataliwa mwezi uliopita, kabla ya sasa kuongeza Pauni 200 milioni na kufanya ifikie Pauni 2 bilioni, ikiwa ni mwanja mrefu unaotosha kabisa kuinunua klabu hiyo.

Katika ofa yake ya mwanzo, Ek alisema kitu ambacho alijibiwa na wamiliki wa Arsenal wa sasa, Mmarekani Kroenke ni kwamba hawana shida ya pesa, lakini anaamini kwa kupandisha dau zaidi linaweza kufanya mchakato huo ukatiki.

Kambi ya bilionea Ek ilisema “Hatuendi kokote hadi hapo tutakapoona hili dili limekamilika.”

Watu wa ndani wa klabu ya Arsenal wamekiri wanatarajia kupokea ofa ya pili ya kuhusu mpango wa kuinunua timu hiyo kwa mujibu wa Daily Mail.

Ek anajaribu kutumia mwanya wa michuano ya European Super League ambayo imewafanya mashabiki wa Arsenal kuwachukia wamiliki wa klabu hiyo kwa sasa ili kufanikisha mpango wake wa kuibeba jumla timu hiyo.

Arsenal walikuwa miongoni mwa klabu sita kubwa za England kuunda uanzishwaji wa michuano hiyo ya Super Cup, ambayo imeshindwa kufanyika baada ya kupigwa na mashabiki na viongozi kila kona.

Ek aliweka mambo hadharani juu ya mpango wake wa kuinunua klabu ya Arsenal, akidai kutakuwa na umiliki wa mashabiki, ambapo watakuwa na mwakilishi kwenye bodi na kutakuwa na hisa za dhahabu kwa mashabiki wa timu hiyo.

Magwiji wa Arsenal, Thierry Henry, Dennis Bergkamp na Patrick Vieira ni miongoni mwa watu muhimu kwenye klabu hiyo wanaounga mkono mpango wa bilionea Ek kuinunua klabu hiyo.

Stan Kroenke, ambaye aliimiliki Arsenal jumla mwaka 2018, amekuwa akikosolewa sana kwa namna anavyoiendeesha klabu hiyo.

Arsenal imekuwa ikiporomoka kwa kasi sana kwenye ubora wake kwa muongo wa karibuni, jambo linalomfanya kocha Mikel Arteta kuwa na wakati mgumu wa kukiboresha kikosi hicho na kukifanya kurudi kwenye kiwango chake kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Mtoto wa mmiliki bilionea Kroenke, Josh, ambaye ndiye mkurugenzi wa klabu, amekuwa na majukumu ya kila siku katika kuhakikisha timu ninasimama vyema na kuwa kwenye ubora wake ikiwamo kuchuana kwenye mikikimikiki ya ubingwa wa Ligi Kuu England.

Baada ya kuwatibua mashabiki kutokana na mpango wa kushiriki kwenye Super League, familia ya Kroenke sasa imepanga kufanya usajili wa nguvu wa kikosi hicho kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi ili kupoza mambo.

Hata hivyo, Ek, amekuwa akipata sapoti kubwa kutoka kwa watu wanaosemwa kuwa wa mpira, akiwamo Henry ambaye alisema:

“Najua kuna watu wengi sana wanasubiri kwa hamu kusikia habari za Arsenal kununuliwa. Ni kweli. Daniel ni shabiki wa Arsenal, hakusema kwa ajili ya kupata umaarufu. Ni shabiki wa Arsenal kwa miaka mingi sana.

“Yupo tayari, naweza kuwaambia hivyo. Ameifuata familia ya Kroenke na ameshakusanya pesa kwa ajili ya kutoa ofa ya kununua klabu. Hili jambo litachukua muda mrefu na si jepesi.

“Kitu ambacho kifahamike tu, Daniel hataachana na mpango huu, ataendelea kusubiri hadi hapo Kroenke watakapoamua kuipiga bei.

“Hii itachukua muda mrefu, ila tunafahamu kitu cha kufanya. Na tunachotaka kusema ni kwamba tutahakikisha tunachukua timu, kama Kroenke watakuwa wasikivu.”