Bernardo Silva, Man City ndo basi tena
Muktasari:
- Silva, ambaye ni raia wa Ureno, amekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya City chini ya Pep Guardiola, akisaidia timu hiyo kurejea katika ubora wake baada ya kushuka kiwango msimu uliopita. Hata hivyo, tayari alishawahi kueleza huu ungekuwa msimu wake wa mwisho.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO na nahodha wa Manchester City, Bernardo Silva anatarajiwa kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu kwa uhamisho wa bure, baada ya kudumu kwa miaka tisa katika kikosi hicho.
Taarifa hiyo imethibitishwa na kocha msaidizi wa timu hiyo, Pep Lijnders, aliyesema Silva anastahili kupewa heshima ya kuagwa kwa namna ya kipekee kutokana na mchango wake mkubwa.
Silva, ambaye ni raia wa Ureno, amekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya City chini ya Pep Guardiola, akisaidia timu hiyo kurejea katika ubora wake baada ya kushuka kiwango msimu uliopita. Hata hivyo, tayari alishawahi kueleza huu ungekuwa msimu wake wa mwisho.
“Bernardo ni mchezaji wa kipekee. Ukikosa uwepo wake hata mechi moja tu unaona tofauti. Fikiria msimu mzima,” amesema Lijnders.
Licha ya mafanikio hayo, Silva amewahi kuonyesha kutofurahia maisha ya England, akisema angependa zaidi kuishi Kusini mwa Ulaya.
“Kama Manchester City ingekuwa Lisbon, ningebaki hadi miaka 40,” aliwahi kusema.
Kwa sasa, klabu kadhaa zinatajwa kuwania saini yake, zikiwemo Juventus, Barcelona pamoja na klabu za ligi ya Marekani (MLS). Pia, aliwahi kuwindwa na Paris Saint-Germain lakini dili hilo halikufanikiwa.
Silva analenga kumaliza safari yake City kwa mafanikio kwa kushinda taji la saba la Ligi Kuu England kabla ya kuondoka rasmi.
Kuondoka kwake, pamoja na uwezekano wa John Stones kuondoka, kutamuacha Phil Foden kama mchezaji pekee aliyesalia kutoka kikosi kilichoweka rekodi mwaka 2018.