Kompany chaguo kuu kurithi mikoba ya Guardiola
Muktasari:
- Mustakabali wa Guardiola katika timu hiyo umekuwa ukizua mashaka licha ya Man City kuendelea na mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England sambamba na Arsenal, ambapo wababe hao wa Etihad wako pointi tisa nyuma ya The Gunners katika msimamo wa michuano hiyo.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER City wameshauriwa kwamba Vincent Kompany ndiye mtu sahihi wa kumrithi Pep Guardiola iwapo kocha huyo Mhispaniola ataamua kuondoka mwishoni mwa msimu huu baada ya kudumu katika kikosi hicho kwa miaka 10.
Mustakabali wa Guardiola katika timu hiyo umekuwa ukizua mashaka licha ya Man City kuendelea na mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England sambamba na Arsenal, ambapo wababe hao wa Etihad wako pointi tisa nyuma ya The Gunners katika msimamo wa michuano hiyo.
Kutokana na kutokuwa na uhakika juu ya kocha huyo, viongozi wa Man City wameshamuomba awaambie mapema juu ya uamuzi wake kabla ya mwisho wa msimu ili waweze kujipanga kwa safari bila uwepo wake.
Guardiola ana mkataba hadi 2027, lakini hali ya kutokuwa na uhakika imeanza kuathiri mipango ya klabu ikiwamo ile ya usajili ambayo amekuwa na sauti kubwa kuamua nyota anaowataka kikosini.
Si hilo tu, lakini wakati klabu hiyo tayari ina wachezaji kadhaa inaowalenga kwenye uhamisho ujao, baadhi yao wanazingatia mustakabali wa Guardiola katika kufanya uamuzi wakiamini kwamba uwepo wake kikosini utawasaidia kufanya kazi na kocha mwenye mbinu nyingi zitakazowasaidia maisha mwao.
Mshambuliaji wa zamani wa Manchester City, Stuart Pearce, alisema Guardiola ana haki ya kuamua mustakabali wake, lakini klabu inapaswa kufanya kila juhudi kumhakikishia kuwapo kwa muda mrefu zaidi, ingawa kwa sasa vigumu, hivyo kocha wa sasa wa Bayern Munich, Vincent Kompany anastahili kuvaa vitu vyake Etihad.
Naye Ray Parlour, nyota wa zamani wa Arsenal anakubaliana na Pearce akisema ingawa kuondoka kwa Guardiola kutaacha ombwe kwa muda Man City, lakini Kompany anaweza kuwasahaulisha mashabiki wa kikosi hicho machungu ya kumkosa kocha huyo.
“Mafanikio aliyoyafanikisha Guardiola kwa City hayana kifani. Atakapoondoka itakuwa ni siku ya kutisha,” alisema Parlour na kuongeza:
“(Kompany) anaifahamu klabu vyema, anajua mashabiki na anaheshimika. Ikiwa ataenda klabu yoyote inapaswa kuwa Man City pekee. Huyu ndiye mtu anayefaa kwa mashabiki wa City.”
Parlour aliongeza kuwa Kompany ameshawahi kucheza na kufundisha klabu nyingine, lakini kuifahamu kwake vyema Man City kunamfanya awe chaguo bora kuiongoza timu hiyo.