Machaguo kibao ya Silva akisepa Man City
Muktasari:
- Mendes kwa sasa yupo bize kukamilisha dili za mastaa kibao anaowasimamia miongoni mwao wanaomalizia mikataba na wengine wanaoongeza, lakini kwa Silva ni wazi kwamba anakwenda kuvuta mkwanja upya kutoka timu atakayojiunga nayo.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO shoka wa Manchester City, Bernado Silva (31), hivi sasa anaweza kuwa anapitia taratibu orodha ya ofa ambazo zimefikishwa mezani kwake na wakala wake, Jorge Mendes, kwa ajili ya kuamua timu atakayoichezea msimu ujao baada ya mkataba wake Etihad kumalizika.
Mendes kwa sasa yupo bize kukamilisha dili za mastaa kibao anaowasimamia miongoni mwao wanaomalizia mikataba na wengine wanaoongeza, lakini kwa Silva ni wazi kwamba anakwenda kuvuta mkwanja upya kutoka timu atakayojiunga nayo.
Silva kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa kwenda kucheza katika klabu kubwa za Ulaya nje ya England, lakini pia anavutia zile za Saudi Arabia ambapo baadhi zimeshaulizia juu ya upatikanaji wake.
Kwa sasa Juventus ndiyo inayotajwa kuwa imewasiliana moja kwa moja na mchezaji huyo, lakini faili na Mendes lina pia Al Ittihad na Al Nassr za Saudia, Valencia na Sevilla za Hispania pamoja na Inter Miami ya Marekani. Hata hivyo, hadi sasa Klabu ya Juventus bado haijawasilisha ofa rasmi kwa kiungo huyo licha ya taarifa kibao kutoka Italia kuitaja kuwa miongoni mwa zile zenye nafasi kubwa kumpata. Silva atapatikana bure mwishoni mwa msimu mkataba wake utakapoisha, na anatarajiwa kuondoka Man City kwani hakuna ofa ya kumuongezea dili jingine ambayo amepewa. Pamoja na utitiri wa klabu unaomtaka timu yake ya utotoni Benfica imefikisha ofa mezani kwake ikitaka kumrudisha nyumbani.
Hata hivyo, dili la kwenda Mashariki ya Kati limeendelea kujadiliwa tangu majira ya joto ya 2023, wakati Al Hilal walipompa ofa ya mshahara wa takribani Pauni 500,000 kwa wiki pamoja na ada ya kusaini ya zaidi ya Pauni 2 milioni. Silva alihusishwa tena na uhamisho huo majira ya joto yaliyopita, lakini aliweka wazi kuwa hakuwa tayari kuondoka Man City mwaka mmoja kabla ya fainali za Kombe la Dunia 2026.
Hata hivyo, kutokana na kwamba bado hajasaini mkataba mpya, inaonekana kuwa safari yake ya miaka tisa katika Uwanja wa Etihad inaweza kufikia mwisho. Iwapo ataichagua Juventus kama kituo chake kijacho, atafuata nyayo za staa mwenzake wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, aliyekwenda Turin 2018 kabla ya kuondoka 2021.
Tangu alipojiunga na City kwa Pauni 43 milioni mwaka 2017, Silva amekuwa mhimili muhimu katika mafanikio ya klabu hiyo, akishinda mataji sita ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya 2023. Amecheza zaidi ya mechi 400 na amechaguliwa mara mbili kwenye Kikosi Bora cha Mwaka cha PFA miaka ya 2019 na 2022.
Silva aliteuliwa kuwa nahodha wa klabu hiyo msimu uliopita kufuatia kuondoka kwa Kyle Walker na Kevin De Bruyne, na amecheza mechi 41 msimu huu za mashindano yote. Kocha wa City, Pep Guardiola, ameweka wazi kuwa angependa sana mchezaji huyo aendelee kubaki Etihad.
Akizungumza Januari, mwaka huu, Guardiola alisema: “Ningependa sana kwa Man City, na pia kwa upande wangu, Bernardo abaki milele. Lakini tumefanya mazungumzo mengi na yeye na ni juu yake kuamua kilicho bora kwake na familia.” Chochote kitakachotokea msimu huu, msimu ujao au hata baada ya miaka 10 ataendelea kuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa waliowahi kucheza katika historia ya klabu hii. Kikosi hicho cha Guardiola kitacheza na Arsenal katika fainali ya Carabao, leo Jumapili, huku pia kikiwa kimefika robo fainali ya FA na bado kina nafasi ya kushinda ubingwa wa ligi.
Nahodha huyo wa City na wenzake watakuwa na hamu ya kurekebisha makosa Jumapili hii, akilenga kushinda taji lake la tano la Carabao katika maisha yake ya soka. Hata hivyo, matumaini ya Silva ya kushinda tena ubingwa wa Ulaya yalizimwa katikati ya wiki baada ya City kutolewa na Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 5-1.