Benn alipa kisasin kibabe, akimzima Eubank JR
Muktasari:
- Eubank alisimama tena lakini mara moja akajikuta chini kwa mara ya pili baada ya Benn kurudi na shambulio kali. Licha ya kuokolewa na kengele ya mwisho, tayari matokeo yalikuwa wazi.
LONDON, ENGLAND: BONDIA Conor Benn amefanikiwa kulipa kisasi mbele ya mpinzani wake, Chris Eubank Jr. katika pambano la uzito wa middle, lililochezwa jana Jumamosi jijini London, England.
Benn alipata ushindi katika pambano hilo la marudiano dhidi ya Eubank Jr. kwa ushindi wa wazi kupitia alama za majaji wote.
Wawili hao walifufua uhasama baina yao kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur, huku Benn akitafuta kulipiza baada ya kichapo alichopata Aprili mwaka huu.
Bahati nzuri ikawa kwa Benn baada ya kufanikiwa kulipa kisasi hicho baada ya kutoa onyesho la hali ya juu kabisa la ndondi, akilitawala pambano lote na kumwangusha Eubank mara mbili katika raundi ya mwisho.
Pambano lilipelekwa kwenye alama za majaji, lakini mshindi alikuwa mmoja tu, Benn aliyetangazwa mshindi akiwa ameandamana na baba yake mzazi, Nigel Benn.
“Safari imekuwa ndefu na nahisi huu ndio mwisho wa simulizi ya Benn dhidi ya Eubank,” Benn alisema baada ya pambano.
“Imekwisha. Hii inafikia tamati hapa. Kila mtu alikuwa anasema siwezi kupigana ndondi, sasa waweke maneno yao mifukoni.”
“Hili halingekuwa hivi bila Chris na bila baba zetu. Hii ni ya vizazi. Hii ni historia. Hongera kwa Chris, sina la zaidi. Si vibaya kwa watoto wawili wa ‘silver spoon’,” alitania.
Benn alianza kwa kasi, akishambulia mara moja ili kuipandisha kelele ya mashabiki, huku Eubank naye akipiga ‘jab’ chache.
‘Next Gen’ a.k.a ya Eubank aliingilia raundi ya pili kwa nguvu na Benn akajikuta chini ya ulingo, jambo lililosababisha mwamuzi kuwaonya wachezaji wote wawili.
Benn aliendeleza kasi yake na wakati mmoja Eubank naye akaanguka chini, ingawa haikuhesabiwa kama ‘knockdown’.
Pambano lilianza kuwa na purukushani kidogo, lakini udhibiti uliendelea kubaki kwa Benn hadi raundi ya sita, ambapo Eubank tena alianguka, japo bado haikuhesabiwa kama ‘knockdown’.
Benn aliendelea kuongeza shinikizo, akipiga ngumi kali ya mkono wa kulia katika raundi ya saba na kumcheka Eubank wakati kengele ilipopigwa.
‘The Destroyer’ (jina la utani la Benn) alimkwamia Eubank katioka kamba na kuendelea kumshambulia kwa mfululizo, huku mpinzani wake akichoka, akijua pambano linaenda kwake.
Katika raundi ya mwisho, Benn aliweka nguvu zote, akipiga ngumi nzito iliyomwangusha Eubank chini.
Eubank alisimama tena lakini mara moja akajikuta chini kwa mara ya pili baada ya Benn kurudi na shambulio kali. Licha ya kuokolewa na kengele ya mwisho, tayari matokeo yalikuwa wazi.