Ben White kukaa nje kwa miezi kadhaa
Muktasari:
- Kuumia kwa White, linakuwa ni pigo kubwa kwa Arsenal juu ya harakati zao za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kwani staa huyu amekuwa tegemeo tangu msimu uliopita.
LONDON, England: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta ameweka wazi beki wao, Ben White atakuwa nje ya uwanja kwa miezi kadhaa kutokana na majeraha.
Kuumia kwa White, linakuwa ni pigo kubwa kwa Arsenal juu ya harakati zao za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kwani staa huyu amekuwa tegemeo tangu msimu uliopita.
“Ben atakuwa nje kwa miezi mingi. Amekuwa na matatizo mbalimbali, hali yake bado haipo sawa na ilifika mahali lazima tumlinde mchezaji. Itachukua miezi kadhaa,” alisema Arteta kuhusu staa huyo ambaye ameumia goti na tayari amefanyiwa upasuaji.
Mchezaji huyo ambaye msimu huu amecheza mechi tisa za Ligi Kuu England majeraha aliyopata yanaweza kumweka nje hadi mwakani.
Kabla ya mchezo wao wa jana, Arsenal ilikuwa inashikilia nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikiwa na mechi zao tano zilizopita ilikuwa imeshinda moja.
Kukosekana kwa White imekuwa ni pigo kubwa kwa Arsenal kwani sio mchezaji pekee ambaye anaumwa kwa sasa, pia Bukayo Saka na Declan Rice hadi kufikia Ijumaa hakukuwa na uhakika wa kucheza dhidi ya Nottingham Forest sawa na ilivyokuwa kwa Leandro Trossard ambaye aliumia alipokuwa akiitumikia timu ya taifa ya Ubelgiji.
Mchezaji mwingine ambaye anahitaji wiki kadhaa kabla ya kuonekana tena uwanjani ni staa wao kutoka Japan, Takehiro Tomiyasu ambaye msimu huu amecheza mechi moja tu kutokana na jeraha la goti.
“Atakuwa nje kwa wiki chache ili kuendelea na matibabu yake. Tomiyasu ni mchezaji anayefanya kazi saa 24 ili kuwa fiti na anajisikia vibaya kuwa nje. Tuna matumaini atapata nafuu,” alisema Arteta kuhusu Tomiyasu.