Beki Guehi analipwa kibosi Man City
Muktasari:
- Beki huyo wa England mwenye umri wa miaka 25 alikamilisha uhamisho wake wa Pauni 20 milioni kutoka Crystal Palace, Jumatatu.
MANCHESTER, ENGLAND: BEKI wa kati, Marc Guehi amekuwa mchezaji wa pili anayelipwa mshahara mkubwa zaidi Manchester City baada ya kujiunga na klabu hiyo.
Beki huyo wa England mwenye umri wa miaka 25 alikamilisha uhamisho wake wa Pauni 20 milioni kutoka Crystal Palace, Jumatatu.
Amesaini mkataba wa miaka mitano na atakuwa akilipwa mshahara wa Pauni 300,000 kwa wiki.
Man City ilikuwa tayari kumpa Guehi dili hilo kubwa kwa sababu ada ya uhamisho aliyolipiwa Palace ilikuwa ndogo, ikizingatiwa kwamba mkataba wake Selhurst Park ulikuwa unaisha mwishoni mwa msimu.
Ni Erling Haaland pekee anayemzidi Guehi kwa mshahara, akiwa analipwa kiasi cha kushangaza cha Pauni 525,000 kwa wiki katika kikosi hicho kinachonolewa na Mhispaniola, Pep Guardiola.
Mshahara wa Guehi wa Pauni 300,000 kwa wiki unalingana na wa Bernardo Silva, huku Omar Marmoush akiwa nyuma yao kwa Pauni 295,000.
John Stones, Gianluigi Donnarumma na Ruben Dias wote wanapokea Pauni 250,000 kwa wiki, kulingana na takwimu za Spotrac.
Tijjani Reijnders (Pauni 230,000), Phil Foden (Pauni 225,000) na Rodri (Pauni 220,000) wote wanapata zaidi ya kiwango cha Pauni 200,000 kwa wiki ambacho Josko Gvardiol analipwa. Chini zaidi ya orodha hiyo, mchezaji mwingine aliyejiunga Januari, Antoine Semenyo, analipwa Pauni 150,000 kwa wiki. Makipa wa akiba Stefan Ortega na James Trafford wanalipwa Pauni 90,000 na Pauni 50,000 kwa wiki mtawalia.
Hii inamweka Trafford katika kiwango sawa na Oscar Bobb, Abdukodir Khusanov na jambo la kushangaza Jeremy Doku.
Wachezaji waliotoka akademi ya klabu, Nico O’Reilly (Pauni 30,000) na Rico Lewis (Pauni 25,000), ndio wanaopokea mishahara midogo zaidi katika kikosi cha kwanza chenye maskani yake Etihad. Man City iliishinda Liverpool katika mbio za kumsajili Guehi.