Bei za tiketi Kombe le Dunia 2026 zavujishwa
Muktasari:
- FIFA ilitangaza siku ya Jumatano kuwa tiketi zingekuwa zinaanza kwa bei ya chini ya Sh146,250, lakini haikutoa orodha kamili ya bei kulingana na kila hatua ya mashindano.
MASHABIKI wa soka wanatarajiwa kugharamika kwa kiasi kikubwa baada ya bei za tiketi za Kombe la Dunia 2026 kuvuja.
FIFA ilitangaza siku ya Jumatano kuwa tiketi zingekuwa zinaanza kwa bei ya chini ya Sh146,250, lakini haikutoa orodha kamili ya bei kulingana na kila hatua ya mashindano.
Hata hivyo, The Athletic imechapisha orodha kamili ya bei ambazo mashabiki wanatarajiwa kukabiliana nazo katika mashindano hayo ya msimu ujao wa joto ambayo yatafanyika Marekani, Canada na Mexico.
Ikiwa timu ya taifa ya England inayonolewa na Thomas Tuchel, ambayo kwa sasa ina rekodi ya asilimia 100 katika mechi za kufuzu itafuzu kwenda katika mashindano hayo, basi mashabiki wa England watakabiliwa na gharama kubwa za tiketi.
Bei ya chini kabisa ya tiketi katika hatua ya makundi itakuwa ni Sh146,250, lakini bei hiyo inaweza kupanda hadi Sh1.4 milioni kwa mechi moja ya hatua hiyo. Bei za tiketi hubadilika kulingana na iwapo moja ya mataifa wenyeji wanacheza na pia uwanja wenyewe.
Kwa mfano, tiketi ya hatua ya makundi kwa mechi ya ufunguzi ya Marekani huko Los Angeles itagharimu Sh574,600, wakati tiketi ya mechi ya Canada huko Toronto itagharimu Sh567,250.
Katika hatua ya mtoano ya timu 32 bora, tiketi itagharimu Sh1.6 milioni. Hatua ya 16 bora, bei itapanda hadi Sh2.2 milioni. Robo fainali bei itapanda hadi Sh4.1 milioni. Nusu fainali, tiketi itakuwa Sh6.7 milioni. Kwa fainali itakayofanyika kwenye Uwanja wa MetLife, bei za tiketi itaongezeka maradufu ambapo itaanzia Sh4.9 milioni hadi Sh15 milioni.
Hii ina maana kuwa shabiki atakayehudhuria mechi zote za hatua ya mtoano katika Kombe la Dunia lijalo anaweza kutumia hadi Sh7.3 milioni kwa tiketi za daraja la nne pekee.
Kwa upande mwingine, gharama ya tiketi za daraja la kwanza kwa mechi zote za mtoano inaweza kufikia hadi Sh30 milioni.
Ufafanuzi huu wa bei za tiketi unakuja baada ya kauli ya Makamu wa Rais wa FIFA, Victor Montagliani, ambaye amesema kuwa baadhi ya mechi huenda zikachezwa baada ya saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki kutokana na wasiwasi wa hali ya hewa huko Marekani.
"Ni changamoto ya kawaida katika ukanda huu, majira ya joto ni ya joto kali nchini Canada na Marekani. Lakini ni muhimu tujifunze kutokana na hayo.
"Tuna mazungumzo ya kila siku na watangazaji wa Ulaya kuhusu viwanja vinavyoweza kutumika saa 9 alasiri, kama vile Atlanta.
"Kwa wazi, kile tunachojaribu kufanya mara baada ya ratiba kutoka mwezi Desemba, ni kuhakikisha mambo hayo yote yanazingatiwa," amesema.