Kisa matokeo, mashabiki Chelsea wachachamaa!
Muktasari:
- Chelsea ilikumbana na kichapo cha pili mfululizo Ligi Kuu England kutoka kwa Brighton wikiendi iliyopita cha mabao 3-1 nyumbani, baada ya kutoka kuchapwa na Manchester United mabao 2-1 ugenini.
LONDON, ENGLAND: MATOKEO mabovu katika mechi mbili mfululizo yamemtibulia Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca kwa mashabiki wengi wakitaka aondoke, lakini mabosi wa mabingwa hao wa Dunia wamesema bado wanamwamini na watamjadili mwisho wa msimu.
Chelsea ilikumbana na kichapo cha pili mfululizo Ligi Kuu England kutoka kwa Brighton wikiendi iliyopita cha mabao 3-1 nyumbani, baada ya kutoka kuchapwa na Manchester United mabao 2-1 ugenini.
Hata hivyo, licha ya kelele hizo za mashabiki, mabosi wa wababe hao wa darajani, wanaamini kocha huyo bado anaweza akatimiza malengo ambayo wamemwekea na anahitaji kuendelea kupewa muda ili kujenga timu na walishawishika sana kutokana na kiwango ilichoonyesha Chelsea katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu.
Mashabiki walikataa utetezi wa Maresca aliyedai timu imepoteza mechi hizo mbili kwa sababu ya kadi nyekundu, wakidai kadi haikuwa sababu bali kocha huyo ameshindwa na hana kiwango cha kuipa mafanikio timu yao.
Hata hivyo, kadi hizo nyekundu za Robert Sanchez na Trevoh Chalobah zinachukuliwa kwa uzito mkubwa na viongozi wa juu wa klabu ambao wanaamini zimechangia sana timu kufanya vibaya.
Akiwa na Chelsea, Maresca amepoteza mechi tano tu katika miezi sita iliyopita na katika mechi hizo, nne kati ya hizo timu hiyo ilimaliza ikiwa pungufu.
Mbali ya masuala ya kadi, matajiri wanaamini timu pia inaangushwa na majeraha ya wachezaji tegemeo na kwa sasa mastaa kama Cole Palmer na Liam Delap ni miongoni mwa wale walioumia.
Moja kati ya malengo ambayo matajiri wa klabu hiyo yenye maskani yake jijini London walimpa Enzo ilikuwa ni kuhakikisha anafanya vizuri katika michuano ya kimataifa jambo ambalo alilitimiza katika Kombe la Dunia la klabu lililofanyika Marekani na sasa mtihani alionao ni kufanya tena vizuri Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Chelsea itakutana na Benfica ya Jose Mourinho leo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya katika Uwanja wao wa nyumbani kabla ya kuivaa Liverpool katika Ligi Kuu England Jumamosi ya wiki hii pia.
Mabosi wa Chelsea wanaamini pia katika mafanikio ya Maresca msimu uliopita na mbali ya kuwa na matatizo na kupitia kipindi cha mpito, aliiwezesha timu kushinda Uefa Conference League na kumaliza nafasi nne za juu kabla ya kuchukua Kombe la Dunia la Klabu.
Hata hivyo, kocha huyu akiendelea kufanya vibaya bado atakuwa katika hatari ya kuonyeshwa mlango wa kutokea kwani licha ya ukweli wamiliki wa timu wanamlinda na kumwamini, mashabiki wengi hawaonekani kuridhishwa naye.