Bayern yaiweka patamu Arsenal kwa Kimmich

Muktasari:
- Kimmich mkataba wake wa sasa utafika tamati mwishoni mwa msimu huu, hivyo anajiandaa kuwa mchezaji huru. Arsenal imetajwa kuwa moja ya timu zinazohitaji huduma ya Mjerumani huyo, ambaye amejipambanua kama mchezaji bora kabisa kwenye Bundesliga.
MUNICH, UJERUMANI: MABOSI wa Bayern Munich wamesema tena kwa msisitizo hawataongeza ofa yao kwa Joshua Kimmich licha ya mazungumzo ya mkataba mpya kukwama.
Kimmich mkataba wake wa sasa utafika tamati mwishoni mwa msimu huu, hivyo anajiandaa kuwa mchezaji huru. Arsenal imetajwa kuwa moja ya timu zinazohitaji huduma ya Mjerumani huyo, ambaye amejipambanua kama mchezaji bora kabisa kwenye Bundesliga.
Amebeba mataji manane ya ligi, matatu ya DFB-Pokals na mwaka 2020 alibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya huku akiwa kwenye kikosi hicho cha Allianz Arena tangu 2015. Mazungumzo ya mkataba mpya baina ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 na mabosi wake wa Bayern yamechukua muda mrefu bila kufika mwafaka.
Lakini, tangu wiki iliyopita, mazungumzo yamekwama na jambo hilo limezifanya timu zinazomtaka Kimmich kuanza mchakato wa kumchukua. Bayern bado ina matumaini mchezaji wao atabaki kwenye kikosi ambacho kwa sasa kipo kwenye nafasi nzuri ya kunyakua ubingwa wa Bundesliga msimu huu.
Kwenye mazungumzo ya karibuni, mabosi wa Bayern walifichua wanamtaka Kimmich abaki, lakini hawataongeza ofa yao waliyoweka mezani kwa mchezaji huyo.
Kimmich anataka mshahara wake anaolipwa kwa sasa, Pauni 320,000 kwa wiki uongezeke. Lakini, Bayern tayari imeshaongeza mishahara kwa wachezaji Jamal Musiala na Alphonso Davies, hivyo hawataki kuingia gharama zaidi.
Gwiji wa Bayern na Ujerumani, Lothar Matthaus alisema Kimmich anapaswa kujipambanua ni kitu gani anataka.