Bayern v Dortmund Hii ni tamu

MUNICH, UJERUMANI. KWANINI derby ya ‘Klassiker’ kati ya Bayern Munich na Borussia Dortmund inaendelea kuwa mechi tamu zaidi ya kuisubiri katika Bundesliga? Hizi hapa ni sababu.

Kwanza msimu huu, karibu kila mjadala ni kuhusu ubora wa Bayer Leverkusen, ambayo imekaa kileleni kwa tofauti ya pointi 10 juu ya mabingwa watetezi Bayern Munich na chama hilo la kocha Xabi Alonso halijapoteza mchezo wowote katika michuano yote Ulaya msimu huu (mechi 38).

Kiufupi, kwa mara ya kwanza katika misimu 12, inaonekana kwamba Bayern haitatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani msimu huu. Lakini bado matumaini ya Leverkusen kubeba taji hilo kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo ilipoanzishwa miaka 120 iliyopita, yatakuwa na nafasi katika mechi hii ya derby ya Ujerumani itakayopigwa Jumamosi Machi 30 kwenye Uwanja wa Allianz Arena unaotarajiwa kufurika mashabiki.

Ikiwa na mataji 32 ya Bundesliga, Bayern inasafiri katika anga la pekee kama klabu yenye mafanikio zaidi nchini Ujerumani. Dortmund, hata hivyo, inafuatia kimafanikio ikiwa imeshinda taji hilo mara tano sawa na Borussia Monchengladbach na, tangu mwanzo wa miaka 1990, ndio imekuwa mpinzani mkubwa wa Bayern.

Kiujumla, tangu Ujerumani Magharibi na Mashariki zilipoungana 1991, ni timu nne tu zilizotwaa ubingwa wa Bundesliga, huku Bayern na BVB zikishinda taji hilo mara 26 jumla kati ya mataji 32 yaliyowaniwa tangu wakati huo. Pia timu hizo pinzani zimetwaa taji la DFB mara 15 katika kipindi hicho, na pamoja na Hamburg, ndio timu pekee za Ujerumani zilizowahi kutwaa ufalme wa soka la Ulaya. Dortmund ilibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1997 na Bayern ikafanya hivyo mara sita katika miaka ya 1974, 1975, 1976, 2001, 2013 na 2020.

“Hizi ndio aina ya mechi zinazokufanya kwanini ucheze soka. Mzuka wa mashabiki unaokuwapo kuizunguka mechi ni wa kipekee,” kiungo wa Bayern, Leon Goretzka alifafanua msimu uliopita alipoulizwa kuhusu kushindana katika mechi za Der Klassiker.

Kocha wa BVB, Edin Terzic, kwa upande wake alichoona kuhusu wapinzani wake ni, “Wanakuwa wakali sana dhidi yetu kuliko wanavyokuwa dhidi ya klabu nyingine za Bundesliga.” 

Kutokana na ugumu wa mechi hiyo, imekuwa sababu ya Der Klassiker kuwa mechi ya kuamua mambo. Kwa ujumla, Dortmund imemaliza katika nafasi ya pili mara saba katika mataji 11 mfululizo ya Bayern, wakati Bayern ilishika nafasi ya pili msimu wa 2011/12 wakati Dortmund ilipotwaa ubingwa wa Bundesliga, ikiwa ndio mara ya mwisho Bayern kutoka mikono mitupu.

Kila mmoja anafahamu umuhimu wa kihistoria wa mechi hii na atataka kushinda, hasa mara hii ambayo, Dortmund inafukuzia nafasi ya Top 4 ya kufuzu Ligi ya Mabingwa na Bayern inataka kudumisha matumaini madogo ya ubingwa.

“Kila shabiki wa soka na kila mwanasoka anaisubiri Der Klassiker,” nahodha wa Bayern, Manuel Neuer alisema, huku kocha wake, Thomas Tuchel, ambaye wakati huo alikuwa Dortmund  - alikiri kwa kusema, “Hii ni mechi kubwa Ujerumani, na ni mechi kubwa kwetu.” 

Hii mechi haivutii ndani pekee, bali hadi kwingineko duniani. Ni kama ilivyo derby ya Real Madrid vs Barcelona; Juventus dhidi ya AC Milan; Liverpool  - Manchester United; Boca Juniors vs River Plate, ukizitaja kwa uchache. 

Straika anayefunga atakavyo Harry Kane na mdunguaji wa hatari Niclas Fullkrug wanatarajiwa kuonyeshana ubabe wakati timu hizo zitakapokutana Jumamosi hii.

Hii sio ya kukosa.