Hawa bado wapo sana Man United

Muktasari:

  • Wakati mashabiki wakisubiri kuona huo usajili mpya na wale watakaoondoshwa, kinachoelezwa kuna mastaa watano, ambao wamekuwa kwenye kiwango bora chini ya kocha Erik ten Hag kwa sasa, wataendelea kubaki, hawataguswa.

MANCHESTER, ENGLAND: Manchester United inatazamiwa kuwa bize sana kwenye dirisha lijalo la usajili, ikipanga kuleta mastaa wapya, huku ripoti zikidai kuna wachezaji wasiopungua 12 watafunguliwa mlango wa kutokea.

Wakati mashabiki wakisubiri kuona huo usajili mpya na wale watakaoondoshwa, kinachoelezwa kuna mastaa watano, ambao wamekuwa kwenye kiwango bora chini ya kocha Erik ten Hag kwa sasa, wataendelea kubaki, hawataguswa.

Hii hapa, orodha ya mastaa watano ambao tajiri Sir Jim Ratcliffe atabaki na huduma zao ili kuleta wengine wa kuja kuwaongezea nguvu ili kupafanya Old Trafford kuwa mahali tishio kwa wapinzani kwa mara nyingine.

1.Andre Onana; Mwanzoni maisha yake yalikuwa magumu, lakini kipa huyo Mcamerooni amekuwa na msaada mkubwa kwenye kikosi cha Man United.

2.Lisandro Martinez; Kukosekana kwake kwenye beki ya timu hiyo kumeonyesha matatizo makubwa ambapo United imekuwa ikiruhusu mabao mepesi sana. Ubora wake unamhakikishia maisha Old Trafford.

3.Kobbie Mainoo; Ameibuka kutoka kwenye akademia ya Man United na tangu alipoanza kupewa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza amekuwa panga pangua. Fundi kabisa.

4.Alejandro Garnacho; Winga kinda, Garnacho, 19, amekuwa kwenye kiwango bora sana msimu huu na bila ya shaka atawekwa kwenye orodha ya wachezaji watakaowania tuzo ya mchezaji bora wa msimu kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.

5.Bruno Fernandes; Ndiye nahodha na anaongoza timu hiyo kwa mifano. Fernandes amefunga mabao 15 msimu huu, ikiwamo manane katika mechi nane za mwisho, huku akiasisti pia mara 11. Unamuachaje sasa!