Bayern Munich, Liverpool zamweka njia panda Wirtz

Muktasari:
- Timu hizi zote zimempa staa huyu ofa nono ya mshahara na zipo tayari pia kutoa kiasi cha ada ya uhamisho kinachohitajika.
KIUNGO mshambuliaji wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz, anatarajiwa kuchagua kati ya kujiunga na Bayern Munich au Liverpool ndani ya siku kumi zijazo.
Timu hizi zote zimempa staa huyu ofa nono ya mshahara na zipo tayari pia kutoa kiasi cha ada ya uhamisho kinachohitajika.
Wirtz amezivutia timu nyingi barani Ulaya kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu msimu uliopita ambapo alicheza mechi 45 za michuano yote, amefunga mabao 16 na kutoa asisti 15.
Awali, staa huyu alihusishwa kuwa katika rada za Manchester City ambayo ilihitaji kumsajili kama mbadala wa Kevin de Bruyne anayeondoka mwisho wa msimu.
Mkataba wa sasa wa kiungo huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Staa huyu amesifika kwa upambanaji na kutokana tamaa.
Rodrygo
ARSENAL inaangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 24, Rodrygo, ambaye ameripotiwa kuwa anahitaji kuondoka katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa sababu haoni kama anapewa nafasi kubwa katika kikosi hicho.
Mkataba wake wa sasa na Madrid unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Kevin De Bruyne
NAPOLI na Chicago Fire zinaongoza katika vita ya kuiwania saini ya kiungo wa kati wa Manchester City, Kevin De Bruyne, 33, ambaye anatarajiwa kuondoka City kama mchezaji huru katika majira haya ya kiangazi.
De Bruyne alitangazwa kuondoka Man City mwishoni mwa msimu huu baada ya mabosi wa timu hiyo kuamua kutompa mkataba mpya.
Luis Diaz
BARCELONA inapambana kwa ajili ya kumsajili winga wa Liverpool na timu ya taifa ya Colombia, Luis Diaz, mwenye umri wa miaka 28, ambaye bado ana miaka miwili katika mkataba wake wa sasa.
Awali, mwaka jana, Diaz aliripotiwa kuwa angejiunga na Barca katika dirisha la majira ya baridi mwaka huu na sababu kubwa ni kwa sababu ni ndoto yake.
James McAtee
KIUNGO wa Manchester City, James McAtee, anawindwa sana na Bayer Leverkusen ambayo imepanga kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiwa Man City itakubali kumuuza.
Licha ya kuonyesha nia ya kutaka kumsajili, hadi sasa bado Man City haijafanya uamuzi wowote juu ya kumuuza staa huyu. McAtee mwenye umri wa miaka 22, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Enzo Fernandez
CHELSEA imesisitiza kwamba haina mpango wa kumuuza kiungo wake wa kimataifa wa Argentina, Enzo Fernandez, licha ya staa huyu mwenye umri wa miaka 24 kuwa kwenye orodha ya wachezaji ambao Real Madrid imepanga kuwasajili katika dirisha lijalo.
Enzo ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2032, amekuwa akiwindwa na Madrid tangu mwaka jana.
Moise Kean
RAIS wa Fiorentina, Rocco Commisso, anatarajiwa kukutana na mshambuliaji wa timu hiyo na Italia, Moise Kean ili kujaribu kumshawishi mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 asalie kwenye kikosi chao baada ya vigogo wengi kuonyesha nia ya kutaka kumsajili. Moise ambaye mkataba wake wa sasa unaisha 2029, msimu huu amecheza mechi 43 na kufunga mabao 21.
Viktor Gyokeres
VIKTOR Gyokeres amewaambia wachezaji wenzake wa Sporting Lisbon kwamba hana uhakika atacheza wapi msimu ujao, licha ya uwepo wa ofa nyingi kutoka timu kubwa barani Ulaya ikiwa pamoja na Arsenal na Manchester United.
Staa huyu wa kimataifa wa Sweden, mkataba wake wa sasa unaisha 2028, msimu huu amecheza mechi 51 na kufunga mabao 53.