Bayer Leverkusen yabeba ubingwa Bundesliga

New Content Item (1)
New Content Item (1)

HUU ni wakati ambao mashabiki wa Bayer Leverkusen wameusubiri kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.

Kutoka kutaniwa 'Neverkusen' hadi kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Ujerumani maarufu kama Bundesliga 'what a moment'.

 Hii ni sawa na mtumwa kutawazwa kuwa mfalme.

Imewezekanaje? Mbele ya Bayern Munich ambao wanaonekana kulitawala soka la Ujerumani kutokana na nguvu kubwa waliyonayo kiuchumi na Borussia Dortmund, huku Leverkusen ambayo msimu uliopita ilikuwa katika hatari ya kushuka daraja hadi kuwa timu tishio.

"Mzee wa mipango, mbunifu". Hayo ni machache kati ya maneno ambayo mashabiki wa Bayer Leverkusen walitumia kumuelezea Xabi Alonso, siku chache kabla ya mechi ya leo.

Chini ya usimamizi wake, klabu hiyo imeweka rekodi nyingi za kibabe ambazo ni kama utukufu kwenye taji la kifalme ambalo wamevalishwa leo, Jumapili baada ya kuwachapa mabingwa wa zamani wa ligi hiyo, SV Werder Bremen.

Kwanini waliitwa Neverkusen? Hilo lilikuwa jina la utani baada ya kukosa taji hilo katika mtindo wa kushangaza mwishoni mwa msimu wa 1999-2000 na 2001-2022, huku kikosi kikiwa na mastaa Michael Ballack, Jose Roberto da Silva Junio 'Ze Roberto', Paulo Roberto Rink na Adam Matysek.

Alonso ndiye kidume ambaye amebadili upepo wa mambo huko Ujerumani kwa Leverkusen ambayo wakati akipewa kibarua cha kuinoa timu hiyo Oktoba 5, 2022, kumrithi Gerardo Seoane hakuna ambaye alikuwa akidhani kuwa pengine msimu unaofuata Mhispania huyo angeweza kufanya balaa hili.

Aliikuta Leverkusen ikiwa nafasi ya pili kutoka mkiani baada ya michezo minane ya Bundesliga, ikiwa na mwanzo mbaya zaidi wa msimu tangu 1979.

Alikuwa na muda mfupi wa kuiandaa timu na mchezo wake wa kwanza ambao ulichezwa siku tatu baada ya kutambulishwa kwake, lakini kwa bahati nzuri Leverkusen iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Schalke 04.

Katika msimu wake huo wa kwanza Alonso alikuwa pia na kibarua cha kubadili mwelekeo wa timu ambayo ilikuwa imesaliwa na mechi tatu katika hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Ulaya.

Baada ya kufungwa mabao 3-0  na Porto kwenye Uwanja wa BayArena Oktoba 12 na kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Atletico Madrid kwenye Uwanja wa Metropolitano Oktoba 26 kisha kutoka suluhu 0-0 dhidi ya Club Brugge nyumbani Novemba mosi, Bayer Leverkusen walimaliza wa tatu katika hatua hiyo hivyo waliangukia katika hatua ya mtoano ya Europa League.

Baada ya miezi michache ya kwanza migumu kwa Alonso, Bayer Leverkusen hatimaye walibadili kiwango huku Alonso akiwaongoza hadi nusu fainali ya kwanza ya Europa baada ya miaka 21, ambapo walitolewa na Roma ambayo  wakati huo ilikuwa ikifundishwa na kocha wake wa zamani wa Real Madrid, Jose Mourinho.

Mwishoni mwa msimu huo, Bayer Leverkusen walimaliza katika nafasi ya sita na kufuzu kwa michuano ya Europa msimu huu. Mei 2023, Alonso alithibitisha kwamba angesalia kwa msimu wa pili licha ya kuhusishwa na Tottenham Hotspur.

Baada ya hesabu za msimu uliopita kumalizika huku akiwa ameifanya kazi ya Leverkusen kikamilifu, mkali huyo wa mipango alijiona kuwa bado ana kitu zaidi ambacho anaweza kufanya na ndio maana aliwagomea Spurs, hivyo aliletewa baadhi ya nyota wa bei 'chee' kulingana na bajeti ndogo waliyonayo ambao aliona wanaweza kuendana na mipango yake.

Nyota hao ni pamoja na Victor Boniface aliyetokea Union Saint-Gilloise ya Ubelgiji na Granit Xhaka kutoka Arsenal kisha wakaanza maandalizi ya msimu huu wakiwa nyumbani, Ujerumani kabla ya kwenda Austria, Hispania na Ufaransa.

Alonso alipata ambacho alikuwa akihitaji katika maandalizi yake kwenye mataifa hayo na msimu ulipoanza kila ambaye alikuwa akisogea alikuwa akichezea na aliyeponyoka katika mikono yao aliambulia sare au suluhu.

Kutoka kuwa timu ambayo ilikuwa katika hatari ya kushuka daraja hadi kucheza michezo 43 bila kupoteza msimu huu hadi kutwaa ubingwa wa Bundesliga ambao ni wa kwanza kwa klabu hiyo tangu kuanzishwa kwake miaka 119 iliyopita.

Leverkusen inabebwa na wachezaji mahiri kama Jeremy Frimpong, Florian Writz, Granit Xhaka, Alex Grimaldo, Amine Adli, Jonas Hofmann ambao wamekuwa na mchango mkubwa wakikipambania kikosi cha Alonso kuhakikisha kinaweka historia kwa mara ya kwanza msimu huu