Barcelona yanogewa na Rashford, kuurefusha mkopo wake
Muktasari:
- Mpango mkakati wa Barca ni kuurefusha mkopo wake kwa mwaka mmoja mwingine, huku ikiendelea kukusanya pesa za kumsainisha mkataba wa kudumu ifikapo mwisho wa msimu.
BARCELONA inapanga kumbakisha mshambuliaji wa kimataifa wa England, Marcus Rashford, 28, kwa mkopo wa msimu mwingine, baada ya huu wa sasa kumalizika, huku ikielezwa ni katika kuepuka kumnunua jumla kwa Pauni 26 milioni zinazotakiwa na Manchester United.
Mpango mkakati wa Barca ni kuurefusha mkopo wake kwa mwaka mmoja mwingine, huku ikiendelea kukusanya pesa za kumsainisha mkataba wa kudumu ifikapo mwisho wa msimu.
Mkataba wa Rashford Man United unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 lakini haonekani kama ana mpango wa kurudi Old Trafford tangu alipotibuana na kocha Ruben Amorim na anatamani kuendelea kukipiga Nou Camp kwani anaamini ndiyo sehemu sahihi kwake baada ya kuonyesha kiwango bora tangu ajiunge nayo.
Tangu kuanza kwa msimu huu, amecheza mechi 38 za michuano yote, amefunga mabao 10 na kutoa asiti 13.
Wilfred Ndidi
MANCHESTER United inaweza kujaribu kumsajili kiungo wa kimataifa wa Nigeria, Wilfred Ndidi, 29, kutoka Besiktas dirisha lijalo. Inaelezwa dili hilo linaweza kuhusisha kubadilishana wachezaji na kipa wao, Altay Bayindir, 27, anaweza kutumika kama sehemu ya makubaliano hayo. Bayindir mwenyewe ameonyesha nia ya kutaka kuondoka kwa sababu hataki kuwa namba mbili, sawa na ilivyo kwa Ndidi ambaye anatamani sana kurudi England.
Jadon Sancho
BORUSSIA Dortmund inaamini inaweza kumshawishi winga wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Jadon Sancho, 25, kurejea kwa mara ya tatu katika kikosi hicho. Sancho ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Aston Villa, mkataba wake na Man United unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na Dortmund inaamini huo utakuwa ni wasaa mzuri wa wao kumsajili kwa sababu hawatolipa gharama yoyote kubwa. Vigogo wa Dortmund bado wanaamini Sancho ambaye amewahi kuonyesha kiwango bora akiwa na kikosi chao ataenda kusaidia sana timu ikiwa watampata kwa msimu ujao.
Sandro Tonali
RIPOTI za ndani zinadai Newcastle watahitaji Pauni 100 milioni katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiwa itaamua kumuuza kiungo wao wa kimataifa wa Italia, Sandro Tonali, 25, katika dirisha lijalo. Inaaminika bei hiyo kubwa inaweza kuwa kikwazo kwa Manchester United, lakini bado wanaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya mchezaji huyo. Tonali ameendelea kuwa miongoi mwa viungo muhimu Newcastle, jambo linaloifanya klabu hiyo kutokuwa tayari kumuachia kirahisi.
Joshua Zirkzee
JUVENTUS imepewa taarifa inaweza kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Uholanzi, Joshua Zirkzee, 24, kutoka Manchester United kwa ada ya takribani Euro 25 milioni katika dirisha lijalo. Mbali ya kupewa ofa ya kumnunua moja kwa moja, Juventus pia inafikiria kutuma maombi ya kumsajili Zirkzee kwa mkopo wa msimu mmoja wenye kipengele cha kumnunua baadaye. Mkataba wa sasa wa Zirkzee unatarajiwa kumalizika mwaka 2029. Staa huyu amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza.
Lamine Camara
KIUNGO wa kimataifa wa Senegal, Lamine Camara, 22, amekuwa mmoja wa mastaa wanaowindwa sana na Newcastle United dirisha lijalo la usajili. Camara kwa sasa anakipiga AS Monaco na inadaiwa ameomba kuondoka mwenyewe kwa ajili ya kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine. Kutokana na uwezo wake na umri mdogo, kiungo huyo anaonekana kuwa uwekezaji wa muda mrefu kwa Newcastle.
Axel Disasi
WEST Ham United inapanga kuanza mazungumzo rasmi na Chelsea ili kumsajili beki wa kimataifa wa Ufaransa, Axel Disasi, 28, kuwa mchezaji wao wa kudumu. Disasi kwa sasa yupo West Ham kwa mkopo, na kiwango chake kimewavutia viongozi wa klabu hiyo wanaotaka kumbakisha kabisa katika kikosi. Hata hivyo, inatarajiwa mazungumzo hayo yatazingatia suala la ada ya usajili. Msimu huu amecheza mechi 21 za michuano yote.
Ricardo Pepi
FULHAM imefikia makubaliano ya awali ya kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Marekani, Ricardo Pepi, 23, kutoka PSV Eindhoven. Taarifa zinaeleza tayari pande zote zimeshafikia makubaliano binafsi juu ya mahitaji ya mshahara kwa mchezaji na bonasi nyingine na kwa sasa kinachojadiliwa ni ada ya uhamisho inayoweza kufikia Pauni 30 milioni.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.