Barcelona yaingia matatani tena
Muktasari:
- Barcelona imejikuta tena katikati ya kashfa ya kifedha, baada ya vyombo vya habari vya El Periodico na polisi wa Kikatalunya (Mossos d’Esquadra) kuripoti dosari kwenye mkataba wa usajili wa Malcom kutoka Bordeaux kwa ada ya euro milioni 42.
BARCELONA, HISPANIA: KLABU ya Barcelona inachunguzwa kwa madai ya kukwepa kodi zinazohusiana na usajili wa winga wa Kibrazili Malcom mwaka 2018. Inadaiwa klabu hiyo ililipa euro milioni 10 kwa mawakala kwa ajili ya “huduma ambazo hazikuwepo,” huku polisi pia wakichunguza aliyekuwa rais wa klabu Josep Maria Bartomeu na baadhi ya viongozi wa zamani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.
Barcelona imejikuta tena katikati ya kashfa ya kifedha, baada ya vyombo vya habari vya El Periodico na polisi wa Kikatalunya (Mossos d’Esquadra) kuripoti dosari kwenye mkataba wa usajili wa Malcom kutoka Bordeaux kwa ada ya euro milioni 42.
Wachunguzi wanadai kuwa Barcelona ililipa Business Futbol Espana (BFE) euro milioni 10 kwa ajili ya “huduma za uwakala” ambazo ama hazikufanyika kabisa au ziliuzwa kwa bei ya juu kupita kiasi.
Malipo hayo, yaliyofanywa kati ya 2018 na 2020, yanadaiwa yalitumika kuficha wajibu wa kodi kwa kubadilisha masharti ya awali ya mkataba wa ajira kati ya klabu na mchezaji. Kwa mujibu wa polisi, mabadiliko hayo yalipunguza kipato kilichoripotiwa rasmi na hivyo kuepuka kulipa kodi halisi inayotakiwa kwa Hazina ya Serikali (Treasury).
Kashfa hii ni sehemu ya uchunguzi mpana zaidi kuhusu mengineyo ya kifedha yaliyofanywa wakati wa uongozi wa Bartomeu. Wengine wanaohusishwa ni Oscar Grau, Jordi Mestre Masdeu, na Francisco Schroder Quijano.
Mwendesha mashtaka anaamini kundi hili lilitumia vibaya fedha za klabu na lilificha matumizi halisi kwa bodi ya uongozi.
Katika uchunguzi mwingine unaohusiana, Bartomeu pia anakabiliwa na mashtaka ya kupokea kamisheni ya euro 30 milioni kutokana na usajili wa Neymar na Antoine Griezmann madai yaliyotolewa kupitia malalamiko rasmi ya rais wa sasa, Joan Laporta.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi wa Mossos, vitendo hivyo vilisababisha hasara ya mamilioni ya euro kwa klabu na wanahisa wake.
Uchunguzi umebaini kuwa mkataba wa awali wa Malcom ulikuwa na malipo ya euro milioni 10 yaliyogawanywa kwa kipindi cha miaka mitatu, lakini baadaye ulibadilishwa kuwa euro 1.5 milioni za moja kwa moja kwa mchezaji na euro 8.4 milioni kupitia kampuni ya BFE.
Polisi wameeleza mabadiliko hayo kama ni “ujanja wa wazi wa kifedha” uliolenga kupunguza kiwango cha kodi ya mapato ya mchezaji (ambayo ilikuwa karibu asilimia 50).
Aidha, waligundua mkataba mwingine ulioitwa “framework agreement” kati ya Barcelona na BFE ulioandikwa kana kwamba ulisainiwa mwaka 2019, lakini kwa kweli ulisainiwa mwaka 2020.
Kati ya ankara 12 zilizochunguzwa, tisa zilionekana hazihusiani na huduma halisi, zikiwa na thamani ya takribani euro 740,000, na zilitajwa kama ankara za uongo zilizotumika kukamilisha malipo ya euro milioni 10 yaliyohusiana na usajili wa Malcom.
Uchunguzi bado unaendelea, na mahakama za Hispania hazijatoa uamuzi kama klabu yenyewe itafunguliwa mashtaka, au kama watakaowajibika ni viongozi binafsi waliokuwa madarakani wakati huo.
Bodi ya sasa inayoongozwa na Joan Laporta imeripotiwa kufanya hatua ya “marekebisho ya kodi ya tahadhari (preventive tax regularization)” ili kuepuka adhabu na kujitenga na mienendo ya kifedha ya uongozi uliopita.